Header Ads Widget

POLISI SITA KUSHITAKIWA KWA MAKOSA YA MAUAJI NA UNYANYASAJI


Wakenya wapatao 15 wameuawa na polisi nchini Kenya katika kipindi hiki ambacho kumewekwa marufuku ya kutembea usiku ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, ripoti huru ya mamlaka inayoangazia makosa ya polisi katika taifa hilo (IPOA) imesema.

Polisi sita sasa watashtakiwa kwa makosa ya mauaji na unyanyasaji, walipohusika katika matukio ya kufyatua risasi dhidi ya raia wakati wakihakikisha marufuku hiyo ya kutotembea usiku inatekelezwa .

Ripoti nyingine ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa , imeandika kuwa kulikuwa na ghasia za polisi katika maeneo mengi ya taifa hilo, katika jamii zipatazo 182, vurugu hizo zilijumuisha kupiga watu, kurushwa kwa gesi ya kutoa machozi , unyanyasaji wa kingono na kuharibu mali za watu.

Matukio mengi makubwa ya vurugu yanahusisha polisi kutumia nguvu katika mji mkuu wa Kenya,Nairobi.

Mtoto mwenye miaka 13 Hussein Moyo aliuawa, Machi 28. Yassin alidaiwa kupigwa risasi tumboni na polisi mjini Nairobi, siku moja tu baada ya marufuku ya kutembea usiku ilipoanza kutekelezwa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Mtoto huyo alikuwa amesimama pamoja na familia yake katika kibaraza cha nyumba yao, orofa ya tatu wakiwa wanawaangalia polisi waliokuwa wakipambana na majirani zao ambao walikuwa hawafuati sheria mpya iliyotangazwa.

Tukio dhidi Yassin ni moja kati ya matukio yaliyothibitishwa na polisi na sasa Mkurugenzi wa mashtaka ya Umma ameidhinisha kukamatwa na kushtakiwa kwa polisi aliyehusika na kitendo hicho.

Msemaji wa Polisi Charles Owino ameiambia BBC kuwa utafiti wa ripoti ya IPOA ni madai na malalamiko tu ya raia na kesi zote ambazo zimetajwa zitahitaji kufanyiwa uchunguzi.

Kwa upande wa kesi ya Yassin, alieleza kuwa kijana yule alipigwa risasi kwa bahati mbaya na polisi wakati afisa huyo wa polisi alipopiga juu kutawanya watu, bahati mbaya risasi ikampata mtoto huyo.

Amesema sio sawa kuwapa Polisi taswira ya 'uuaji' wakati huu walkiwa wanatimiza wajibu wao wa kuhakikisha watu wanafuata utaratibu wa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Serikali inasema imewekeza mamilioni ya fedha katika kuboresha huduma ya polisi tangu mwaka 2007/8 baadha ya ghasia za uchaguzi ambazo zilisababisha mauaji ya watu zaidi ya 1,000 na wengine 300,000 kuondoka katika makazi yao. 

Polisi walishutumiwa kwa kusababisha mauaji ya watu 400.

Lakini wakosoaji wanasema mabadiliko ni kidogo sana - na watu waishio kwenye makazi duni kama wa Mathare wanataka haki yao.