Header Ads Widget

WAKULIMA WA UFUTA SASA KUUZA MAHALI POPOTE ILI KUPATA BEI NZURI




Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge akizungumza wakati alipowatembelea wakulima wa zao la ufuta wilayani Bahi

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ameruhusu wakulima wa zao la ufuta mkoani humo ambao bado wana ufuta nyumbani, kuuza mahali popote ambapo wanaona watapata bei ya kuwafaa.
Dkt. Mahenge ametoa maelekezo hayo ya serikali akiwa wilayani Bahi alipowatembelea wakulima na wafanyabiashara wadogo wa zao hilo baada ya wakulima hao kuiomba serikali kuingilia kati bei ya zao hilo kufuatia kuporomoka kwa bei katika mnada ulioendeshwa Juni 24 mwaka huu ambapo bei ilishuka hadi shilingi 1,250 kwa kilo kutoka shilingi 1,931 katika mnada ulioendeshwa Juni 02,mwaka huu. 

“Maelekezo yangu baada ya kukaa kikao juzi na wafanyabiashara na Wakuu wa Wilaya wote ni kwamba kuanzia sasa, mwananchi yeyote ambaye bado ana ufuta nyumbani aende akauze anakoona yeye kunafaa, hakutakuwa tena na hii zuia zuia isipokuwa tu utatulipia ushuru wetu kwenye geti, mmenielewa ndugu zangu,” amesema Dkt. Mahenge na kuongeza

“Waambieni wananchi wote kwamba muda uliobaki serikali imeamua kuwaachia wananchi wafanye juhudi zao, kama unamuuzia mfanyabiashara muuzie kama unapeleka mwenyewe mjini peleka, lakini kama ipo chini ya tani moja unapeleka bila malipo ikizidi tani moja unalipa ushuru.”

Dkt. Mahenge ameeleza kuwa zipo sababu tatu zilizosababisha kushuka bei ya ufuta kwa kasi mkoani humo ambapo ni athari ya ugonjwa wa Corona ambapo wanunuzi wakubwa duniani bado nchi zao hazijafungua mipaka hivyo imekuwa vigumu kupeleka ufuta katika nchi hizo.

Sababu nyingine ni kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu (2020) mavuno yalichelewa kuanza na wakulima wakajikuta wanaanza kuvuna mwezi Mei na Juni ilhali mikoa ya kusini nayo ndiyo msimu wa kuvuna zao hilo na hata katika nchi za Malawi na Ivori Coast nazo ndiyo msimu wa mavuno, hivyo ufuta kuwepo mwingi sokoni.

Dkt. Mahenge ameainisha sababu nyingine kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020 uzalishaji wa ufuta ulikuwa mkubwa kwani wakulima wamevuna vizuri kwa kuwa mvua zimenyesha vizuri na za kutosha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa katika mnada uliofanyika Juni 24 mwaka huu, wilaya hiyo ilikuwa na tani 78.2 ambapo mnunuzi aliyejitokeza alinunua kwa shilingi 1,250 kwa kilo moja jambo ambalo halikuwaridhisha wakulima na kuamua kutouza shehena hiyo.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kuona kuwa tumeshafanya minada miwili na huu wa leo ni wa tatu na bei haituridhishi kwa sababu tulianza na bei ya 1,820 tulikataa, tukaja 1, 520 nayo tulikataa na hii ya leo ya shilingi 1,250 imekuwa mbaya zaidi, hivyo kama kiongozi baada ya kuona hali inakuwa mbaya nikachukua hatua kwa kushirikiana na wakulima kutafuta mnunuzi nje ya mnada na ambapo tumempata na atachukua mzigo huo kwa shilingi 1,400 na wakulima wameridhia.” amesema Munkunda.

Naye Tito Chifungo, mkazi na mkulima wa ufuta katika Kijiji cha Mundemu ameishukuru serikali na kuridhika na jitihada ilizochukua katika kushughulikia suala hilo hali ambayo kwa niaba ya wakulima wenzie wameridhishwa na uamuzi wa serikali kuruhusu kuuza zao hilo mahali popote wanapopataka.

Kwa mara ya kwanza zao la ufuta mkoani Dodoma limeingizwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani lakini kutokana na kushuka kwa bei serikali imeruhusu wakulima kutafuta masoko na kuuza badala ya kutumia mfumo huo.