Header Ads Widget

GARI LA HALMASHAURI USHETU LAUA, KUJERUHI WATUMISHI


Muonekano wa gari la Halmashauri ya Ushetu Land Cruiser lenye namba za usajili SM 12482 baada ya kupata ajali

Na Damian Masyenene -Shinyanga
Mtumishi mmoja wa Halmashauri ya Ushetu wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Stanslaus Njau (45) amefariki dunia katika ajali ya gari la halmashauri hiyo iliyotokea Mei 31, 2020 saa 3:20 usiku katika eneo la D4N barabara ya Kahama-Isaka baada ya kuacha njia na kupinduka.

Mbali na Njau ambaye ni dereva aliyekuwa analiendesha gari hilo, ajali hiyo ilimsababishia majeraha ya mguu wa kushoto, Afisa Kilimo wa halmashauri hiyo, Mapenzi Mshana (53) ambaye amelazwa katika hospitali ya Mji Kahama kwa matibabu zaidi na hali yake inaelezwa kuendelea vizuri.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni Mosi, 2020 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, amelitaja gari lililopata ajali kuwa ni Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili SM 12482 mali ya halmashauri ya Ushetu, huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni mwendokasi.

“Gari hilo likiwa linatokea Kagongwa kuelekea Kahama mjini liliacha njia, kupinduka na kusababisha kifo kwa dereva na majeruhi mmoja wote watumishi wa halmashauri ya Ushetu, gari husika lipo kituo cha polisi Kahama na majeruhi amelazwa katika haspitali ya halmashauri mji wa Kahama akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea nzuri. 

“Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo ukisubiri ndugu kwa taratibu za mazishi, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi kwahiyo natoa wito kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali,” amesema Kamanda Magiligimba.
Picha zote kwa hisani ya Shaban Njia