Header Ads Widget

ACT WAZALENDO CHAONESHA NIA YA KUUNGANA NA CHADEMA UCHAGUZI MKUU 2020


Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu

CHAMA Cha ACT-Wazalendo kimesema kipo tayari kuungana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mwezi Oktoba mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi zake ndogo zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam jana ambapo alisema kuwa wanahitaji ushirikiano wa vyama vya upinzani vyenye malengo thabiti ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani na kuleta mabadiliko kwenye maisha ya wananchi.

Shaibu alisema tayari wamekiandikia barua Chadema kuhusu nia ya chama chake kuunga mkono juhudi zozote za kuunganisha nguvu katika uchaguzi huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Watanzania walio wengi.

“Mara baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kutangaza kufungua milango ya ushirikiano wa vyama, siku iliyofuata nilimwandikia barua ya kupokea hatua hiyo kwa mikono miwili na kuonyesha utayari wa ACT-Wazalendo katika suala hilo muhimu.

“Tunajua CCM haipendi umoja wa vyama vya upinzani, itafanya kila njia kutugawanya, na sisi ACT Wazalendo tupo tayari kwa umoja na tutalisimamia hilo kwa nguvu zote”alisema Shaibu.

Aidha mapema wiki iliyopita, Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika kilitangaza kukaribisha majadiliano ya ushirikiano na vyama vinavyotaka kushirikiano nacho.

Mnyika alisema Chadema kinafungua milango miwili muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, ambapo aliutaja mlango wa kwanza kuwa wanaufungua kwa watia nia wote wa urais na mlango mwingine niwa majadiliano na vyama ambavyo vina dhamira ya kweli ya kushirikiana katika uchaguzi huo.

Chanzo: Mtanzania Digital

SOMA ZAIDI>>>
https://mtanzania.co.tz/act-wazalendo-tutaungana-na-chadema-uchaguzi-mkuu/TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807