Header Ads Widget

KATIBU MKUU WA ZAMANI YANGA SC AFARIKI DUNIA




Klabu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam imepata pigo baada ya kuondokewa na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wake, Lawrence Mwalusako ambaye amefariki leo Mei 25, 2020 Asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mjomba wa marehemu, Augustino Mwakyembe mchezaji huyo alikuwa anasumbuliwa na Kiharusi.

Taarifa ya kifo cha Mwalusako imethibitishwa pia na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania, Mussa Kisoki ambapo amesema kuwa Mwalusako alikuwa amelazwa baada ya kufanyiwa upasuaji, ambapo taratibu za kuchukua mwili zinaendelea na msiba huo utakuwepo Ubungo Jijini Dar es Salaam, familia itatoa taarifa rasmi baada ya taratibu zote kukamilika.

Mbali na nafasi ya ukatibu mkuu ndani ya Yanga, marehemu Mwalusako aliwahi pia kukipiga ndani ya Wanajangwani hao ambao alijiunga nao mwaka 1985 na kuichezea pia timu ya taifa (Taifa Stars).

Kabla ya kujiunga na Yanga SC, Mwalusako alitokea Pan African kama kijana ambae bado yuko shuleni na alikuwa beki hatari wa kulia na kushoto na pia alikuwa anapanda, baadae aliichezea klabu ya Waziri Mkuu ya Dodoma kisha kujiunga na Yanga ambapo alistaafu mwaka 1990 baada ya kuichezea Chuo Kikuu kwa muda.

Mwalusako aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa kwanza wa kuajiriwa Yanga SC mwaka 2009 akichukua nafasi ya Lucas Kisasa.

Shinyanga Press Club Blog inaipa pole familia ya Lawrence Mwalusako na Wana Yanga wote!