Header Ads Widget

AMERIKA YA KUSINI YAONGOZA KWA MAAMBUKIZI YA CORONA.


Shirika la afya duniani WHO limesema kitovu cha maambukizi ya virusi vya corona sasa kipo katika nchi za Amerika Kusini baada ya takwimu kuonyesha kuna kasi kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo katika eneo hilo.

Kutokana na kulipuka kwa maambukizi zaidi kwenye nchi za Amerika Kusini na ya kati, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona duniani kote sasa inakaribia milioni 5.2 na watu zaidi ya 337,000 wameshakufa. Nchini Brazil pekee idadi ya watu waliokufa imepindukia watu 20,000. Watu wengine 310,000 wameambukizwa nchini humo. Sasa nchi hiyo inashika nafasi ya tatu duniani kwa maambukizi, ikizifuatia Marekani na Urusi.
Mkururugenzi wa kitengo cha hali ya dharura kwenye shirika la afya duniani Mike Ryan amethibitisha kwamba Amerika ya Kusini sasa imekuwa kitovu cha maradhi ya Covid -19. Ameeleza kuwa wameshuhudia kuongezeka kwa maambukizi katika nchi nyingi za Amerika Kusini, hata hivyo amesema Brazil ndiyo iliyoathirika zaidi kwa sasa.

Tofauti na barani Ulaya na Marekani ambako wazee ndiyo walioathirika zaidi, nchini Brazili idadi kubwa ya  watu waliokufa walikuwa vijana waliojikuta katika hali ya kulazimika kufanya kazi licha ya hatari ya maambukizi. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka chuo kikuu cha Brasilia Mauro Sanchez amesema watu wengi wanajiweka katika hatari ya kupata maambukizi kwa sababu hawana njia nyingine. Wachimba makaburi katika mji wa Sao Paulo wamesema wanalemewa na kazi ya kuzika kutokana na idadi kubwa ya vifo.
Wakati huo huo nchini Marekani rais Donald Trump anayedhamiria kutafuta njia ya kuondokana na mgogoro wakati ambapo anakabiliwa na changamoto ya kutaka kuchaguliwa tena, ameongeza shinikizo kwa serikali za majimbo na za mitaa ili kulegeza hatua za karantini. Janga la corona limeuathiri uchumi wa Marekani kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba miito inatolewa juu ya kulegeza hatua hizo licha ya kuongezeka kwa maambukizi. Watu zaidi ya Milioni 1.6 wameambukizwa virusi vya corona nchini humo na zaidi ya watu 96,000 wameshakufa 
Chanzo ni 👇
https://m.dw.com/sw/amerika-ya-kusini-sasa-yaongoza-kwa-maambukizi-ya-corona/a-53546125
TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807