Header Ads Widget

AJUZA WA MIAKA 111 APONA VIRUSI VYA CORONA


Baada ya kupona virusi vya corona Juana Zúñiga anatarajia kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwake miaka 112 iliyopita

Akiwa na umri wa miaka 111 Juana Zúñiga amekuwa ndiye mgonjwa mzee zaidi nchini Chile kupona virusi vya corona, maafisa kutoka taifa hilo la Amerika ya Kusini wanaeleza.


Bi Zúñiga alikutwa na ugonjwa huo baada ya kutokea mlipuko wa maambukizi katika kituo cha kulea wazee ambacho anatunzwa.

Hakuathirika sana na virusi hivyo licha ya kuwa na matatizo katika mfumo wake wa upumuaji hata kabla ya mlipuko wa corona.

"Hakuonesha dalili yeyote, japo alipatwa na homa mara chache jambo ambalo lilikuwa zuri," ameeleza Bi María Paz Sordo ambaye ni mkurugenzi wa kituo kinachomhifadhi ajuza huyo.

Bi Sordo ameeleza pia kuwa iliwabidi wamhamishe Bi Zúñiga ambaye pia anafahamika kama Juanita, katika eneo lengine la kituo hicho ili kumtenga na wakaazi wengine.

"Kumuondoa katika eneo alilolizoea ndio lilikuwa jambo gumu zaidi."

Juanita amekuwa akiishi katika kituo hicho katika jiji la Santiago kwa miaka sita sasa, toka alipofiwa na dada yake ambaye alikuwa akiishi naye nyumbani.

Mwezi Aprili, wahudumu saba wa kituo hicho pamoja na wakaazi 18 - akiwemo Juanita - walikutwa na maambukizo ya corona.

Juanita alitengwa katika wodi maalumu kwa siku 28, na kuhudumiwa na maafisa wa wazee kutoka serikalini.

Bi Juaniti ni mwenyeji wa mji wa pwani wa Valparaíso. Hana mtoto na hakuwahi kuolewa, anatarajia kutimiza miaka 112 mwezi Julai.

Chile ina zaidi ya wagonjwa 82,000 waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona, ambapo zaidi ya watu 800 wamefariki.