Header Ads Widget

MWANAFUNZI WA UDOM MBARONI KWA KUSAMBAZA MTANDAONI UONGO KUWA DAWA YA COVID 19 NI KUNYWA NA KUJIPAKA PILIPILI NA UPUPU


Na Amon Mtega - Songea 
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)Ibrahimu Bukuku (26)kwa tuhuma za kusambaza ujumbe unaodaiwa kuwa ni wa upotoshwaji kwenye mitandao ya kijamii uliohusu dawa ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Akizungumza ofisini kwake jana Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa katika kijiji anachoishi cha Lunyele (Darpori) kata ya Tingi Wilaya ya Nyasa mkoani humo.

 Kamanda Maigwa amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza Chuo Kikuu cha Dodoma anayesomea shahada ya Sayansi fani ya Biolojia (Bachelor of Science in Biology) amesambaza ujumbe kupitia simu yake ya kiganjani usemao 'Dawa ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona ni kutumia upupu pamoja na pilipili.

Maigwa amefafanua kuwa ujumbe huo ambao umesambazwa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii ya Whatsap kuwa "Dawa ya Covid 19 ni kuchukua pilipili kichaa sufuria moja iliyotwangwa halafu changanya na maji vikombe vitano kisha kunywa kutwa mara saba kwa muda wa siku tatu na siku ya nne chuma upupu na kujipaka mwili mzima" jambo ambalo linadaiwa kuwa upotoshwaji mbele za jamii na linachukuliwa mchezo kwenye gonjwa hili la Covid 19.

 Amesema kuwa jeshi la Polisi litaendelea kuwatafuta wale wote wanaofanya mchezo na ugonjwa huu wa Covid 19 unaosababishwa na Virusi vya Corona na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kujibu mashistaka yanayowakabili.
CHANZO - MATUKIO DAIMA TV

Post a Comment

0 Comments