` TRA, CHINA KUJA NA MIFUMO YA KISASA KURAHISISHA BIASHARA

WANDAMAN HOTEL

TRA, CHINA KUJA NA MIFUMO YA KISASA KURAHISISHA BIASHARA

    


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Taasisi ya Forodha ya China (General Administration of Customs of China – GACC), ukiongozwa na Naibu Waziri wa Taasisi hiyo, Bw. Wu Humping, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za forodha baina ya nchi hizo mbili.

Katika mazungumzo hayo, pande hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya mifumo ya kisasa ya forodha, kubadilishana uzoefu na utaalamu wa kiteknolojia ili kuongeza ufanisi wa shughuli za forodha, kurahisisha taratibu za uondoshaji wa shehena na kupunguza muda wa kufanya biashara katika mipaka.

Ushirikiano huo unalenga pia kuboresha usimamizi wa taarifa za forodha, kuimarisha udhibiti wa mizigo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara, hatua itakayosaidia kupunguza vikwazo vya kibiashara na kuweka mazingira rafiki zaidi ya biashara kati ya Tanzania na China.

Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuongeza ufanisi wa mifumo ya forodha nchini, kurahisisha biashara ya kimataifa na kuhakikisha huduma za forodha zinaendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa, huku zikichangia kukuza biashara, uwekezaji na mapato ya Taifa.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464