📌 Utafiti wabaini asilimia 94 ya wafanyabiashara wana mapato yanayozidi gharama za biashara zao.
📌 Aziagiza taasisi za fedha kubuni mikopo inayokidhi mahitaji halisi ya wafanyabiashara wadogo.
📌 Azitaka mamlaka za udhibiti kuweka mazingira rafiki kwa ubunifu wa huduma za kifedha na kulinda watumiaji.
📌 Awahimiza wafanyabiashara kutunza kumbukumbu sahihi na kusimamia vizuri fedha za biashara.
DAR ES SALAAM
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo (Mb), amezindua ripoti ya utafiti wa wafanyabiashara wadogo uliolenga ya ufuatiliaji wa shughuli za kila siku za wafanyabiashara wadogo ili kubaini hali zao za kifedha na kibiashara kwa ujumla.
Akizindua ripoti hiyo iliyoandaliwa na taasisi ya FSDT. Mhe Londo amesema licha ya ripoti hiyo kuchambua mwenendo wa biashara, usimamizi wa fedha na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kibiashara, itasaidia kuzalisha takwimu zitakazosaidia serikali na taasisi za kifedha kujua mahitaji halisi ya wafanyabiashara wadogo hususani wanawake na vijana.
Amesema ripoti hii imekuja kwa wakati muafaka kwani hivi karibuni serikali ilizindua Sera ya maendeleo ya jasirimali ndogo na za Kati hiyo itasaidia uwepo wa taarifa za utafiti huu itasaidia kwa serikali kuweka mkakati mazuri wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa Kati.
Katika hafla hiyo, Mhe. Londo amesema utafiti huo utasaidia Serikali kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na kati sambamba na mkakati wa biashara na hivyo kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani wenye thamani ya Dola za Marekani Trilioni Moja.
Amesema utafiti umebaini kuwa asilimia 94 ya wafanyabiashara wana mapato yanayozidi gharama za biashara zao, licha ya mapato hayo kubadilika kati ya mwezi mmoja na mwingine huku asilimia 38 hutegemea akiba binafsi na asilimia 33 hukopa kwa ndugu na marafiki wanapokabiliwa na changamoto za kifedha huku Katika matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, asilimia 72 ya miamala bado hufanyika kwa fedha taslimu, huku asilimia 40 wakitaja gharama kubwa za huduma hizo na asilimia 31 wakikabiliwa na changamoto ya ujuzi wa kuzitumia.
Aidha Mhe Londo ameongeza kuwa biashara zinazomilikiwa na wanaume katika utafiti huo hupata faida kwa wastani wa asilimia 73 zaidi ya zile zinazomilikiwa na wanawake huku matokeo hayo yakimpelekea Mhe Londo kutoa wito kwa taasisi za fedha kubuni mikopo yenye masharti ya marejesho yanayozingatia mzunguko na hali halisi ya mapato ya wafanyabiashara wadogo, pamoja na kupanua upatikanaji wa mikopo ya muda mfupi, bima na huduma nyingine za kifedha sambamba na taasisi za fedha na watoa huduma za teknolojia kuboresha mifumo ya malipo ya kidijitali ili iwe rahisi na nafuu, huku mamlaka za udhibiti zikitakiwa kuweka mazingira rafiki kwa ubunifu wa huduma za kifedha na kulinda watumiaji na kuwawezesha wanawake kupata mitaji, ujuzi wa usimamizi wa fedha na taarifa za masoko, na kuwataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu sahihi na kusimamia vizuri fedha za biashara zao.
Awali akizungumzia utafiti huo Mtendaji mkuu wa FSDT Eric Masinda amesema utafiti huo umefanyika kwa kipindi cha miezi 14 chini ya uongozi wa Kamati ya Kitaalam iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Deogratias Macha na ulifuatilia shughuli za kila siku za wafanyabiashara wadogo ili kuelewa hali zao halisi za kifedha na kibiashara, ikiwemo mapato na matumizi, usimamizi wa fedha, upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha, matumizi ya malipo ya kidijitali pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika biashara.
Amesema Jumla ya vituo vitano vya biashara nchini ambavyo ni Mutukula (Kagera), Kahama (Shinyanga), Namanga (Arusha), Tunduma (Mbeya) na Kariakoo (Dar es Salaam) vilitumika kwa ajili ya utafiti huo kwa kushirikiana na Trademark Africa (TMA), Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), huku ukipata ufadhili na uungwaji mkono wa Gates Foundation na Trademark Africa.
Wizara ya Viwanda na Biashara ilikuwa miongoni mwa wadau walioshiriki kutoa mchango wa kitaalamu na kusimamia utekelezaji wake, kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, vyama vya wafanyabiashara na taasisi za kifedha na matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kusaidia Serikali na taasisi za kifedha kuboresha sera, kanuni na mifumo ya huduma za kifedha ili kukidhi mahitaji halisi ya wafanyabiashara wadogo na kuimarisha ukuaji wa biashara zao nchini.
















