

Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Shinyanga.
Na Greyson Kakuru – Shinyanga Press Club.
Benki ya CRDB inatarajia kuadhimisha mashindano ya baiskeli kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Novemba 14, 2026, kwa kufanya Tamasha la Mbio za Baiskeli litakaloambatana na hamasa ya uchangiaji damu salama kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji wa damu katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Novemba 9, 2026, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, amesema mashindano hayo yameandaliwa na Benki ya CRDB kupitia Tawi la Shinyanga, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Shinyanga Yetu, Damu Yetu.”
Amesema tamasha hilo litahusisha washiriki zaidi ya 200 watakaoshindana katika makundi matatu, ambapo kundi la kwanza litakuwa la wabobevu wa mchezo wa baiskeli watakaokimbia umbali wa kilomita 150 kutoka Shinyanga hadi Isaka.
“Tamasha la Mbio za Baiskeli litapambwa na mashindano ya mbio za baiskeli zenye washiriki zaidi ya 200 watakaogawanyika katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni la wabobevu wa baiskeli watakaokimbia kilomita 150 (Shinyanga–Isaka), ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya pesa taslimu kiasi cha shilingi milioni 2,mshindi wa pili milion 1.5 na mshindi wa tatu-milion 1 na huku washindi wa nne hadi kumi wakipatiwa nauli,” amesema Wagana.
Ameeleza kuwa kundi la pili litakuwa la vijana chipukizi (Amacha), watakaokimbia kutoka Uwanja wa Kambarage hadi Tinde, ambapo mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi milion 1,mshindi wa pili -laki 5 na mshindi wa tatu-laki 3 na washindi wa nne hadi kumi wakipatiwa nauli ya ushiriki.
Aidha, kundi la tatu litakuwa la wanawake, ambao watazunguka Uwanja wa CCM Kambarage mara 20 wakiwa na ndoo za maji kichwani, huku mshindi wa kwanza akipata zawadi ya shilingi laki 8,mshindi wa pili laki 5 na mshindi wa tatu -laki 3 na washindi wa nne hadi kumi wakipatiwa nauli ya ushiriki.
Wagana amefafanua kuwa kupitia tamasha hilo, Benki ya CRDB inalenga kukuza michezo na kutangaza huduma zake kwa washiriki pamoja na wadau mbalimbali watakaoshiriki.
Amesema wadau watakaoshiriki ni pamoja na Chama cha Baiskeli Tanzania, Jeshi la Polisi na wananchi kutoka maeneo mbalimbali, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
“Katika tamasha hili pia kutakuwa na ngoma na nyimbo kutoka kwa wasanii mbalimbali na sanaa nyingine nyingi zikishuhudiwa na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani,” ameongeza Wagana.

Meneja wa Biashara wa Kanda ya Magharibi, Anselm Mwenda akizungumza na vyombo vya habari.
Naye Meneja wa Biashara wa Kanda ya Magharibi, Anselm Mwenda, amewahimiza wakazi wa Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani kujitokeza kushiriki tamasha hilo ili kupata burudani na kufurahia wiki njema huku wakipata fursa ya kufahamu na kutumia huduma za Benki ya CRDB.
Kwa upande wake, Mratibu wa Damu Salama katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Joel David Mbale, amesema wananchi watapata fursa ya kuchangia damu salama katika zoezi litakaloambatana na tamasha hilo, hatua inayolenga kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaohitaji damu.

.jpg)

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464