Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa agizo la kuondolewa kwa mfumo wa mnunuzi mmoja wa zao la pamba kuanzia msimu ujao, ili kuwapa wakulima uhuru wa kibiashara na kuchagua wanunuzi katika soko.
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, katika ziara yake ya kukagua shughuli za Serikali mkoani humo.
Amesema mfumo wa mnunuzi mmoja wa zao la pamba hauleti tija kwa uchumi na biashara ya wakulima, kutokana na gharama za uzalishaji wanazotumia huku maamuzi kuhusu bei ya soko yakisimamiwa na mnunuzi mmoja.
“Serikali imepokea changamoto yenu na kuanzia msimu ujao soko la pamba hakutakuwa na mnunuzi mmoja na wakulima wapate uhuru wa kuamua wauze kwa nani katika soko hilo,” amesema Mwigulu.
Wakulima wa pamba walipokea kauli hiyo kwa shangwe, wakionesha kufurahishwa na uamuzi huo wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Nchemba amekemea uzembe kwa baadhi ya watumishi wa umma wanaoshindwa kuzingatia miongozo ya Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi, kwa kufanya kazi kwa mazoea na kuwapa usumbufu wananchi wa hali ya chini.
“Tusiufanye uzembe kuwa sheria na taratibu katika kazi zetu, ni vema kutimiza majukumu yetu kwa kumsaidia Rais Samia katika kutimiza ahadi zake kwa wananchi,” amesema Mwigulu.
Pia amesema Serikali inachukua hatua kuhusu bei ya saruji nchini kwa kuondoa kodi ya saruji inayoagizwa kutoka nje pamoja na malighafi zinazotumika kutengeneza saruji.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Lucy Mahenga, aliwasilisha hoja za wananchi kuhusu changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa barabara ya Kolandoto hadi Mhunze, kutofanya kazi kwa Kiwanda cha Shirecu kilichopo Mhunze na ukosefu wa mitandao ya maji katika vijiji saba vya jimbo hilo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
