WAZIRI MKUU DK. MWIGULU NCHEMBA AAGIZA USANIFU UPYA WA BARABARA YA KOLANDOTO–KISHAPU
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, ameagiza ufanyike upy usanifu wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga kwenda Kishapu, ili kuondoa adha wanazokabiliana nazo wananchi wa wilaya hiyo kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Ametoa agizo hilo leo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kishapu katika mkutano wa hadhara.
Amesema, usanifu wa barabara hiyo ulifanyika tangu mwaka 2017, hivyo ameagiza ufanyike upya na kuingizwa katika mipango ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha, ili ijengwe kwa kiwango cha lami.
“Usanifu wa barabara hii ufufuliwe upya na kuingizwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha ujao,” amesema Waziri Mkuu Nchemba.
Katika hatua nyingine, amepiga marufuku ununuzi wa pamba wilayani humo kufanywa na kampuni moja pekee, akitaka kuwepo kwa kampuni nyingine, ili kuongeza ushindani na fursa kwa wakulima.
Pia, amekemea tabia ya kukamata pikipiki na bajaji, akielekeza badala yake wahusika watozwe faini kwa mujibu wa sheria badala ya vyombo hivyo vya usafiri kurundikwa vituo vya Polisi.
Aidha, amezungumzia suala la kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi hususan saruji, akisema serikali tayari imechukua hatua za kukabiliana na hali hiyo kwa kufuta kodi ya uagizaji wa saruji kutoka nje ya nchi pamoja na kodi ya malighafi zinazotumika kutengeneza saruji.
Awali, Waziri wa Ujenzi Masanja Kadogosa, akizungumzia barabara hiyo ya Kolandoto–Kishapu, amesema usanifu wake ulifanyika mwaka 2017, na kwamba serikali itaufanyia upya, kisha kuiingiza barabara hiyo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.
Naye Mbunge wa Kishapu Lucy Mayenga, awali alizungumzia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo na kumuomba Waziri Mkuu asaidie kuzitatua.
Miongoni mwa kero alizozitaja, ni ubovu wa miundombinu ya barabara ya Kolandoto–Kishapu, ukosefu wa maji safi na salama, kufa kwa viwanda vya SHIRECU Kishapu, pamoja na malalamiko ya wakulima kuhusu ununuzi wa pamba unaofanywa na kampuni moja pekee.
Waziri wa ujenzi Mhe. Masanja Kadogosa
Mbunge wa Jimbo la kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



