` SERIKALI KUZIFANYIA KAZI HOJA NANE ZA KUIMARISHA BIASHARA YA KABONI

WANDAMAN HOTEL

SERIKALI KUZIFANYIA KAZI HOJA NANE ZA KUIMARISHA BIASHARA YA KABONI


Serikali imeahidi kuyafanyia kazi mapendekezo nane yaliyowasilishwa na wadau wa mazingira na biashara ya kaboni mwishoni mwa maadhimisho ya Wiki ya Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania (Tanzania Climate Week 2026) jijini Dodoma, ikiwa ni hatua inayolenga kuimarisha sekta hiyo, kuvutia wawekezaji na kuongeza manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kufunga jukwaa hilo lililohitimishwa Ijumaa, Novemba 27, 2026, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesisitiza kuwa serikali itayachukua maazimio hayo kwa uzito mkubwa huku akisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa vitendo na ufuatiliaji wa karibu ili yasiishie kwenye makabrasha.
Mapendekezo hayo yanajikita katika kuimarisha uratibu wa kitaifa wa masuala ya tabianchi na kujenga jukwaa thabiti la makubaliano ya pamoja, pamoja na kuongeza uwezo na rasilimali za Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ili kiweze kusimamia ipasavyo soko linalokua kwa kasi.


Aidha, wadau wamependekeza kutatuliwa kwa changamoto za kodi na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika biashara ya kaboni, kuharakisha utekelezaji wa Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris, na kuwezesha jamii pamoja na serikali za mitaa kushiriki kikamilifu na kunufaika na miradi ya kaboni.
Hoja hizo pia zinahimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, kuunganisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu wa jamii, na kutumia tafiti pamoja na ushahidi wa kisayansi kama msingi wa maamuzi ya kisera.


Akiwasilisha mapendekezo hayo, Mkurugenzi wa Idara ya MRV katika Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Dkt. Deo Shirima, amesema hatua hizo ni nyenzo muhimu katika kujenga mazingira wezeshi yatakayohakikisha biashara ya kaboni inachochea maendeleo ya kiuchumi sambamba na uhifadhi endelevu wa mazingira, huku takwimu zikionyesha kuwa NCMC imesajili miradi 117 ya kaboni na takriban miradi sita tayari imeanza uzalishaji na kuleta mapato.




Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, amebainisha kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kuendeleza biashara ya kaboni, mifumo ya ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu, uwekezaji wa kijani na nishati jadidifu, kupitia jukwaa lililoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na NCMC na Serikali ya Norway ili kufungua fursa pana za masoko ya kaboni.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464