` DKT. SAJAD RAI ANG'ARA, ATUNUKIWA TUZO YA MAISHA YOTE KWA MCHANGO SEKTA YA MAFUTA

WANDAMAN HOTEL

DKT. SAJAD RAI ANG'ARA, ATUNUKIWA TUZO YA MAISHA YOTE KWA MCHANGO SEKTA YA MAFUTA

 

Meneja Mkazi wa Kampuni ya Moil Industries Dkt. Sajad Habib Rai akionesha tuzo ya Mchango wa Maisha Yote (Lifetime Achievement Award) aliyotunukiwa na Taasisi ya Mikono Tanzania jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2026, kwa kutambua mchango wake katika sekta ya nishati ya mafuta nchini Tanzania.
****

Meneja Mkazi wa Kampuni ya Moil Industries, Dkt. Sajad Habib Rai, ametunukiwa tuzo ya Mchango wa Maisha Yote (Lifetime Achievement Award) na Taasisi ya Mikono Tanzania, kutambua mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya nishati ya mafuta nchini Tanzania.

Tuzo hiyo imetolewa Novemba 27, 2026, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya tuzo za Top 100 Executive List zilizowakutanisha viongozi, wakurugenzi, mameneja na watendaji wakuu kutoka taasisi na kampuni mbalimbali za umma na binafsi ndani na nje ya nchi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Sajad amesema kutambuliwa kwake ni hatua nyingine kubwa katika safari yake ya utumishi na mchango wake katika sekta ya mafuta, akibainisha kuwa siku moja kabla ya hapo alipokea tuzo nyingine iliyotambua mchango wake katika sekta hiyo.

"Namshukuru Mungu kwa hatua hii kubwa, lakini pia nitumie nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa tuzo hizi kwa kuona mchango ninaoutoa kwa kampuni yangu na Taifa langu katika eneo hili la nishati ya mafuta. Ninaahidi kuendelea kutumia weledi wangu kuleta mabadiliko chanya," amesema Dkt. Sajad.

Dkt. Sajad ni mbunifu wa mfumo wa udhibiti wa mafuta unaojulikana kama BIL, unaolenga kupunguza mianya ya udanganyifu katika uagizaji na ununuzi wa mafuta, hatua inayochangia kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo na kuongeza mapato ya Serikali.

Ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji na viongozi wa taasisi mbalimbali kutumia nafasi walizonazo kuleta ubunifu, tija na mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kazi kwa manufaa ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mratibu na Mwanzilishi wa tuzo hizo, Deogratius Kihwele, amewapongeza washindi wote na kuwataka viongozi na watendaji wakuu wa kampuni na taasisi nchini kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu, weledi na uadilifu ili kuleta matokeo chanya katika taasisi wanazoziongoza.

"Top 100 Executive List si tuzo za kutambua mafanikio ya mtu mmoja mmoja, bali ni jukwaa la kuthamini uongozi bora, ubunifu na mchango wa watendaji wakuu katika kukuza taasisi, kampuni na uchumi wa Taifa. Hivyo, rai yangu ni kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuweka mikakati itakayozalisha matokeo chanya na maendeleo endelevu," amesisitiza Kihwele.

Tuzo hizo ni sehemu ya utaratibu wa kila mwaka unaoendeshwa na Taasisi ya Mikono Tanzania kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa viongozi na watendaji mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.

Waandaaji wametangaza pia mipango ya kuandaa tuzo nyingine za viongozi wa kimataifa zitakazofanyika mwakani jijini Dubai.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464