` MANISPAA YA SHINYANGA YAZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI, YAPANDA 1,500

WANDAMAN HOTEL

MANISPAA YA SHINYANGA YAZINDUA KAMPENI YA UPANDAJI MITI, YAPANDA 1,500

 


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imezindua kampeni ya upandaji miti katika msimu wa mvua wa mwaka 2026/2027, ambapo jumla ya miti 1,500 imepandwa kwa lengo la kutunza na kuhifadhi mazingira, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo, Novemba 20, 2026, katika Boma la Zahanati ya Ibinzamata.

Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga, amesema kampeni hiyo inalenga kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki katika kufikia lengo la Serikali la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka katika kila halmashauri.
“Kampeni ya kupanda miti milioni 1.5 inalenga kupanda miti katika msimu wa mvua,” amesema Manjerenga.

Aidha, amesema wameandaa mfumo wa kidijitali wa GAS wenye uwezo wa kutoa takwimu za miti iliyopandwa, ikiwamo aina ya miti na maeneo ilikopandwa, kwa lengo la kufuatilia ukuaji wake.
Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Afisa Tarafa ya Samuye, Aron Laizer, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema wilaya nzima ya Shinyanga inatarajia kupanda jumla ya miti milioni tatu katika msimu huu wa mvua.

Amesema miti ina faida nyingi katika kulinda na kuhifadhi mazingira, ikiwamo kuongeza rutuba kwenye ardhi na kusaidia kuimarisha usalama wa chakula.
Baadhi ya wananchi, viongozi na wanachuo walioshiriki katika zoezi hilo, akiwamo Beata Dionis, wamesema wamefurahishwa na kampeni hiyo na kutoa wito kwa jamii kushiriki katika kupanda na kutunza miti.

Aidha, wamewataka wananchi kuacha tabia ya kukata miti ovyo kwa ajili ya kupata kuni na mkaa, badala yake wahamie kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464