

Na Joachim Nyambo,Mbarali
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeahidi kulifanyia kazi ombi la wazee wilayani huo waliotaka kundi hilo kushirikishwa kwa kuwa na wawakilishi kwenye vyombo vya maamuzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli alitoa ahadi hiyo alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani zilizofanyika kiwilaya katika Kata ya KongoloMswiswi.
Mweli alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika jamii na itaendelea kutoa kipaumbele katika huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo huduma za afya na pia maombi na ushauri wanaoutoa.
Alisema ushirikishwaji wa wazee ni muhimu kutokana na uzoefu na busara walizonazo, ambao unaweza kusaidia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya jamii.
Awali Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Michael Sanga akisoma risala ya wazee aliomba wazeekupewa nafasi ya kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kuanzia katika ngazi za kata hadi halmashauri wakisema kundi hilo limesahaulika na halishiriki kama yalivyo makundi ya wanawake,vijana na walemavu.
“Tunaomba wazee washirikishwe katika vikao vya maamuzi, kuanzia Kamati za Maendeleo za Kata hadi vikao vya Halmashauri, ili tupate fursa ya kutoa mawazo na kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii.” Alisema Sanga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo wilayani humo, Hezron Kapwela, aliwataka vijana kutumia nguvu na uwezo walionao kujijengea maisha bora mapema, ikiwemo kujenga nyumba na kujiandaa kwa maisha ya uzeeni.
Kapwela alisema vijana wanapaswa kuanza maandalizi ya maisha ya baadaye wakiwa bado wana nguvu za kufanya kazi, ili kupunguza utegemezi kwa watoto wao wanapofikia uzee.
“Tunawaasa vijana jengeni nyumba mkiwa bado mna nguvu, msije mkawa kama wazee wanaolalamika sasa hivi kwamba watoto hawanijengei nyumba, wakati yeye alianza kuwa na nguvu na nguvu zimepotea sasa anaanza kutishia kutoa laana kwa watoto, hiyo laana hata Munguhaipokei,” amesema Kapwela.”
.jpg)


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464