Katika kuendelea kusogeza karibu zaidi na wananchi huduma za kodi, Mkuu wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro Mhe. Dastan Kyoba amezindua Kliniki ya Kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupatiwa huduma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwenye mji wa Ifakara amesema Kliniki hiyo inaendelea kutoa huduma kwenye ofisi za TRA wilaya ya Kilombero zilizopo Ifakara kwa kutoa huduma zote za kodi ikiwemo kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao.
Amewataka wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kupata huduma hiyo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika katika eneo hilo na imetokana na ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alipotembelea wilayani hapo na kuwasikiliza walipakodi.
"Tumieni fursa hii inayotokana na maelekezo ya Kamishna Mkuu wa TRA ambaye alitutembelea na kuwasikiliza na kuagiza kuwekwa kambi maalum ya huduma za kodi ili changamoto mlizoziwasilisha kwake na nyingine mlizonazo zipatiwe majibu hivyo msipoteze hiyo fursa", amesema Mhe. Kyoba.
Aidha amewasisitiza wananchi umuhimu wa kudai risiti kwa kila manunuzi wanayofanya ili wachangie maendeleo ya nchi kwani miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inahitaji fedha za walipakodi.
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro Bi. Husna Nyange amesema wameanza kwa kusikiliza changamoto za walipakodi na kuzitatua papo kwa hapo ambapo wapo wataalam wa sekta zote muhimu za kodi wanaotoa majibu kwa changamoto za walipakodi.
Amesema kila mwananchi atakayefika katika eneo hilo atapatiwa huduma anayoihitaji sambamba na elimu ya kodi.





