` POLISI WATOA ELIMU KWA WANAFUNZI SHYCOM, KUJIEPUSHA UHALIFU, MAPENZI YA JINSIA MOJA, DAWA ZA KULEVYA

WANDAMAN HOTEL

POLISI WATOA ELIMU KWA WANAFUNZI SHYCOM, KUJIEPUSHA UHALIFU, MAPENZI YA JINSIA MOJA, DAWA ZA KULEVYA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga, limewataka wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), kujiepusha na vitendo vya uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, ulevi, mapenzi ya jinsia moja, na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, likieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha usalama wao na kuathiri masomo yao.
Wito huo umetolewa leo, Oktoba 26, 2026, na maafisa wa Jeshi la Polisi walipofika chuoni hapo kutoa elimu kwa wanafunzi hao wanaoanza masomo, kupitia kampeni ya ongea na wanafunzi wanaoripoti vyuoni kuanza masomo, inayolenga kuwajengea uelewa wa kujilinda na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu maisha na ndoto zao.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga Fraterine Tesha, amesema elimu hiyo imelenga kuwasaidia wanafunzi kutambua madhara ya kujiingiza katika vitendo visivyofaa na kuepuka kuviiga wanapokuwa chuoni.
Amewataka pia, kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao na kutokubali kushawishiwa kujiingiza katika misimamo isiyofaa inayoweza kuwafanya waichukie Serikali.

“Tunatoa elimu hii, ili msije kujiingiza kwenye mambo mabaya na kuharibikiwa mkiwa hapa chuoni, tabia ambazo hamkutoka nazo nyumbani kwenu,” amesema Tesha.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga (OCD), Stephen Kimaro, amewataka wanafunzi hao kujiepusha na vitendo vya uhalifu, ikiwamo kuibiana kompyuta mpakato (laptop), ubakaji, ulawiti na kusambaza picha chafu kwenye mitandao ya kijamii.

Amesema, ni jukumu la kila mwananchi kulinda mali za umma kwa mujibu wa Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akiwataka wanafunzi hao kuzingatia elimu waliyopewa.
“Mwanafalsafa Sir Robert Peel, katika kanuni ya saba, anasema polisi ni wananchi na wananchi ni polisi. hivyo, ni jukumu la kila Mtanzania kulinda mali zake na za watu wengine,” amesema Kimaro.

Aidha, amewataka wanafunzi hao kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu kwa kutoa taarifa wanapobaini vitendo vya kihalifu, huku akiwasisitiza kutokujichukulia sheria mkononi wala kushiriki katika matukio ya vurugu.
Baadhi ya wanafunzi hao, akiwamo Salama Salumu, wamesema elimu waliyopewa, imewasaidia kuelewa namna ya kujilinda na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao wanapokuwa chuoni na wakati wa masomo yao.

Mbali na elimu kuhusu uhalifu na matumizi ya dawa za kulevya, wanafunzi hao pia wamepewa elimu kuhusu makosa ya mtandaoni na usalama barabarani.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Shinyanga Fraterine Tesha akizungumza.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga (OCD), Stephen Kimaro akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464