` WAZIRI SANGU AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA SAUDI ARABIA, WAJADILI NJIA ZA KUKUZA AJIRA ZA WATANZANIA

WANDAMAN HOTEL

WAZIRI SANGU AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA SAUDI ARABIA, WAJADILI NJIA ZA KUKUZA AJIRA ZA WATANZANIA

 


Na: OWM (KAM), Dodoma

Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, zimejipanga kuimarisha juhudi katika kutafuta na kukuza fursa za ajira kwa Watanzania nje ya nchi, hususan katika soko la ajira la Saudi Arabia.

Amesema hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu baada ya kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said, leo Semptemba 1, 2026 Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho, Waziri Sangu amesema mikakati inayowekwa na Serikali ili kuimarisha sekta ya ajira hususan ajira za nje ya nchi imesaidia ongezeko la marejesho ya fedha (remittances) zinazotumwa nchini na wafanyakazi wanaofanya kazi ughaibuni na hivyo kuwezesha ukuaji wa  uchumi wa wafanyakazi hao na Taifa kwa ujumla.

Vilevile, amesema Serikali imeandaa mwongozo wa kuratibu shughuli za  Mawakala binafsi wa ajira nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa shughuli za kuwaunganisha watafuta kazi ndani na nje ya nchi zinakuwa na tija.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said amemwakikishia Waziri Sangu kuwa, ubalozi utaendelea kusaidia katika kutambua fursa zaidi za ajira  nchini Saudi Arabia ambazo Watanzania wanapaswa kuzichangamkia.

Kupitia kikao hicho Waziri Sangu pamoja na Balozi Zena walijadili mikakati ya kukuza ajira zaidi kwa Watanzania nje ya nchi pamoja na kusimamia haki na maslahi ya wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya Tanzania. 


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464