
WAZIRI Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema ni muhimu vyama vya siasa viwaunganishe Watanzania badala ya kuwagawa.
Warioba alitoa rai hiyo kabla ya kuanguka ghafla wakati akiwahutubia wadau katika mkutano wa kitaifa ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafakari hali ya siasa nchini.
Kiongozi huyo, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo uliohusisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na wadau wa maendeleo, alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa nchi na kuonya kuwa kuendelea kuwagawa wananchi kwa misingi ya dini, ukanda, Uzanzibari au Utanganyika hakutarudisha amani hata kama nguvu kubwa itatumika.
Muda mfupi baadaye, Mwenyekiti wa TCD, Dorothy Semu, aliwatoa hofu wadau kuwa Jaji Warioba alikuwa akiendelea vizuri na walimruhusu aende kupumzika, wakati viongozi wengine akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, wakihimiza majadiliano ya kisiasa yajikite kwenye hoja zenye maslahi ya taifa badala ya vurugu na mabishano.
Katika mkutano huo huo, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, alieleza kuwa siasa zinabadilika kulingana na wakati na kwamba mijadala ya wadau inapaswa kujikita katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili Taifa, ikiwemo suala la Katiba mpya na kulinda mshikamano wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Naye Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, alisisitiza haja ya ushirikiano wa pamoja katika kuandika historia mpya itakayopeleka nchi mbele, huku Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, akithibitisha utayari wa chama hicho kushirikiana na vyama vingine na asasi za kiraia kupata maridhiano ya kitaifa ili kulinda utulivu wa nchi.
Kauli hizo ziliungwa mkono na wanasiasa wengine akiwemo James Mbatia aliyewataka viongozi kuwa na utashi wa kisiasa na kutumia lugha za staha, wakati Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatib Ali, akisisitiza kuwa wakati wa kunyoosheana vidole umekwisha na sasa ni wakati wa kujenga taifa kwa pamoja.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464