
Mwezeshaji wa mafunzo Elizabeth Mweyo kutoka Manispaa ya Shinyanga
Na Stella Herman,Shinyanga
WALEZI na wasimizi wa vituo vya kulea watoto wadogo Mchana (Daycare) Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kutambua programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto PJT-MMMAM ili kuwaweka watoto kwenye ukuaji wenye utimilifu.
Hayo yameelezwa na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Shinyanga Elizabeth Mweyo ambaye alikuwa mwezeshaji katika semina ya siku mbili kwa walezi na wasimamizi hao zaidi ya 20 iliyoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la ICS kwa lengo la kuwajengea uwezo na utambuzi wa programu hiyo kwa umuhimu wake.
Mweyo amesema katika vituo wapo walezi wapya na wengine wazamani hivyo wanatakiwa kutambua PJT-MMMAM na kuzingatia kundi la watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi minane kwa utafiti uliofanyika watoto hao ubongo wao unaendelea kukua na hata kwenye vituo vya kulea watoto mnao wenye kuanzia umri wa miaka miwili hadi minne.
"Katika programu Jumuishi tunaangalia nguzo tano muhimu ambazo zinamuwezesha mtoto kabla ya kuzaliwa na baada ili kuendelea kukua katika utimilifu wake ambavyo ni lishe,afya bora,Malezi yenye Mwitikio.Ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama"alisema Mweyo.
Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo ambaye alikuwa mwezeshaji katika mada ya huduma za ulinzi. na usalama wa mtoto amesema vipo viashiria vinavyoonyesha mtoto kufanyiwa vitendo vya ukatili na kituo lazima kiwe na kamati inayojumuisha wazazi na kisifanye kazi zaidi ya masaa 12 wala kulaza watoto (boarding) .
Afisa Programu kutoka Shirika la ICS Lucy Maganga alisema katika utekelezaji huu wamekuwa waratibu na kufanya mambo mawili ya kuimarisha mifumo na uchechemuzi na vituo vya kulea watoto ni mojawapo ya kujengewa uwezo.
Mwenyekiti wa vituo vya kulea watoto mchana Manispaa ya Shinyanga Damari Molles amesema semina hiyo imekuwa ni fursa kwao kuongeza ubora kuleta ufanisi katika vituo kwa walezi na wasimamizi kwa kuhakikisha watoto wanakua kwenye hali nzuri.
Daniel Mboto msimamizi wa kituo cha kulea watoto alisema programu jumuishi baada ya kutolewa maelezo ya kina ameweza kuielewa hivyo matarajio ni kwenda kutekeleza kwa vitendo kwa watoto kwa kuzingatia miongozo na misingi ya ukuaji ubongo kwa mtoto.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Rueben ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua semina hiyo alisema wanatambua vituo vinapokea watoto wenye umri wa miaka miwili hadi minne na mnawa andaa kiakili na kimwili na ndiyo maana mnasisitizwa kuwapa lishe bora yenye makundi ya aina tano za vyakula.
Reuben amesisitiza kwenye maeneo ya vituo kuwepo mazingira safi na salama, maeneo ya kupumzikia, matundu ya vyoo yenye uwiano ,kutambua umuhimu wa chanjo kwa watoto na kuwaelimisha wazazi ikiwemo vituo kuvisajili kwa mujibu wa sheria,taratibu na miongozo.
Lucy maganga afisa programu kutoka shirika la ICS

Damari Molles Mwenyekiti wa vituo vya kulea watoto mchana Manispaa ya Shinyanga

Afisa ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo







