Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma, David Majanjala amewasihi viongozi wa ngazi zote kuongoza kwa kutumia hekima ili kufanikisha maono waliyonayo na kuepusha migogoro katika jamii.
Akizungumza juzi jijini Dodoma kwa niaba ya Kiongozi Mkuu wa chama hicho taifa, Dorothy Semu, wakati wa uzinduzi wa vitabu viwili vilivyoandikwa na Dk Daniel Mwangili vinavyoitwa Uongozi Bila Kiti na Kinyume cha Mkondo.
Majanjala alieleza kuwa taifa au familia yoyote inaweza kuangamia endapo kutakuwa na ukosefu wa hekima kwa wanaoongoza au wanaoongozwa. Aliwakumbusha viongozi kujitambua na kutumia nafasi zao kuongoza wengine, huku akiwataka Watanzania kuacha tabia ya kulalamika na kusengenya, badala yake wajikite katika kazi.
Aidha, aliwahimiza vijana wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi za uongozi kwani siasa inagusa maisha ya kila siku ya jamii.
Akizungumzia kazi yake, mtunzi wa vitabu hivyo, Dk Daniel Mwangili, alieleza kuwa lengo la kuandika kazi hizo ni kuhamasisha utamaduni wa kusoma miongoni mwa Watanzania na vijana ili kujiongezea maarifa na kuondoa woga wa kufanya mambo makubwa.
Alisema ukosefu wa utamaduni wa kusoma vitabu husababisha jamii kukosa maarifa na ujasiri wa kusonga mbele kimaendeleo, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji uthubutu wakati uongozi unahitaji maadili yanayotokana na kujisomea na kujiongezea uelewa
