` TCAA NA MAMLAKA ZA VIWANJA VYA NDEGE: TOFAUTI IKO WAPI?

WANDAMAN HOTEL

TCAA NA MAMLAKA ZA VIWANJA VYA NDEGE: TOFAUTI IKO WAPI?

  

Mara nyingi kumekuwa na mkanganyiko kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), huku baadhi ya watu wakidhani kuwa taasisi hizo zinafanya kazi zinazofanana. Hata hivyo, kila taasisi ina majukumu yake mahsusi, ingawa yote yanachangia katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga nchini inakuwa salama, yenye ufanisi na inayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Historia ya usafiri wa anga Tanzania inaanzia kabla ya Uhuru, wakati huduma za usafiri wa anga zilipokuwa zikisimamiwa kupitia taasisi za pamoja za Afrika Mashariki. Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Tanzania iliendelea kujenga na kuimarisha mfumo wake wa kitaifa wa usimamizi wa usafiri wa anga kupitia mageuzi mbalimbali ya kisheria na kiutawala.

Leo, TCAA ndiyo taasisi yenye jukumu la kusimamia sekta ya usafiri wa anga nchini kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga, Sura ya 80. Majukumu yake yanahusisha usimamizi wa usalama, ulinzi na uchumi wa sekta ya usafiri wa anga, pamoja na utoaji wa huduma za uongozaji ndege.

Katika kutekeleza jukumu hilo, TCAA inahakikisha kuwa watoa huduma mbalimbali katika sekta ya usafiri wa anga wanazingatia sheria, kanuni, taratibu, viwango na masharti ya leseni zao. Hii inahusisha mashirika ya ndege, waendeshaji wa viwanja vya ndege, watoa huduma za ardhini, vituo vya matengenezo ya ndege, taasisi za mafunzo ya anga pamoja na wadau wengine wa sekta.
Kwa upande mwingine, TAA ina jukumu la kuanzisha, kuendeleza, kuendesha, kusimamia na kutunza viwanja vya ndege vilivyo chini ya mamlaka yake Tanzania Bara. Pia inaratibu shughuli mbalimbali zinazofanyika katika viwanja hivyo na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa yanayotakiwa.

Kwa upande wa Zanzibar, majukumu ya kuendesha, kusimamia, kutunza na kuendeleza viwanja vya ndege vya Serikali yanatekelezwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA).

Ni muhimu pia kufahamu kuwa TAA na ZAA ni miongoni mwa watoa huduma wanaosimamiwa na TCAA katika masuala yanayohusu usalama, ulinzi na uzingatiaji wa viwango vya usafiri wa anga. Watoa huduma wengine wanaosimamiwa na TCAA ni pamoja na mashirika ya ndege, viwanja binafsi, wamiliki wa viwanja vya ndege kama TANAPA, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na TAWA, pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma katika sekta hiyo.

Kwa ufupi, TCAA inasimamia sekta ya usafiri wa anga, wakati TAA na ZAA zinaendesha, kusimamia, kuendeleza na kutunza viwanja vya ndege vilivyo chini ya mamlaka zao.

Ingawa taasisi hizi zina majukumu tofauti, majukumu hayo yanakamilishana katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na mfumo wa usafiri wa anga ulio salama, wenye ufanisi na unaozingatia viwango vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464