` MATUNDA YA AWAMU YA SITA: VETA KUZINDUA SIMU YA ‘UJUZI Pro’

WANDAMAN HOTEL

MATUNDA YA AWAMU YA SITA: VETA KUZINDUA SIMU YA ‘UJUZI Pro’


Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi umeanza kuzaa matunda yanayoonekana kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ikiongozwa na mafanikio makubwa katika uvumbuzi wa kiteknolojia, uzalishaji, na kukuza ujuzi kwa nguvukazi ya taifa.

Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore, alieleza kuwa mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho kabisa za kuingiza rasmi sokoni simu ya mkononi ya kwanza ya kizalendo iitwayo Ujuzi Pro, hatua iliyofikiwa baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu na kupata kibali rasmi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jambo ambalo ni kielelezo tosha cha uwezo wa wataalamu wa ndani unaochochewa na mazingira wezeshi ya serikali.

Sambamba na hilo, mafanikio hayo yameonekana katika kukuza ujuzi viwandani kupitia ushirikiano na viwanda 16 uliowezesha kutoa mafunzo maalum kwa wafanyakazi 600 na kuongeza tija mahali pa kazi, pamoja na kuwawezesha wananchi 4,465 wakiwemo wajasiriamali wa sekta ya uvuvi kupitia mafunzo yaliyogharamiwa na serikali.

Veta pia imeendelea kuboresha mitaala yake kwa kuandaa mitaala mipya 29 inayokidhi mahitaji ya soko la ajira, ikiwemo ya sekta ya vioo na alumini pamoja na usimamizi na urejelezaji wa taka.

Katika kukuza ubunifu na teknolojia, mamlaka imeratibu bunifu zaidi ya 120 kutoka kwa wanafunzi na wakufunzi, ambapo bunifu 17 zimeshaboreshwa na kuingizwa sokoni kwa ajili ya kuzalishwa kwa wingi, huku mfumo wa kidijiti wa Fundi Connect ukianzishwa ili kuwasajili mafundi rasmi na kuwaunganisha na wateja.

Mafanikio haya yanathibitisha kwa vitendo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga uchumi unaotegemea maarifa, teknolojia na viwanda.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464