Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, akizungumza wakati wa Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga, lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, akizungumza wakati wa Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga, lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Picha na Kadama Malunde 

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, akizungumza wakati wa Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga, lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) Mkoa wa Shinyanga yametakiwa kubadili mtazamo wa uendeshaji kwa kuwekeza zaidi katika ubunifu, ubia na vyanzo vya ndani vya fedha, ili kuhakikisha huduma kwa jamii zinaendelea hata wakati ufadhili kutoka nje unapopungua au kusitishwa.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 3, 2026, na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Pili Hassan Mnyema, wakati akifungua Kongamano la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga, lililofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu: “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali; Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”
Lyamongi amesema kwa miaka mingi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa washirika muhimu wa Serikali katika kuchangia maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, zikiwemo afya, elimu, uwezeshaji wa wanawake na vijana, mazingira, haki za binadamu, ustawi wa jamii na kupunguza umaskini.
Hata hivyo, amesema mabadiliko katika upatikanaji wa ufadhili pamoja na ushindani wa kupata fedha za miradi vinapaswa kuwa kichocheo kwa mashirika hayo kubuni mifumo mipya ya kuhakikisha taasisi zao zinaendelea kuwa endelevu.
“Je, tunaweza kuendelea kutegemea chanzo kimoja cha fedha? Je, tuna mikakati ya kuhakikisha shughuli zetu zinaendelea hata pale ufadhili wa nje unapopungua au kusitishwa? Je, tunatumia ipasavyo rasilimali na fursa zinazopatikana ndani ya Mkoa na nchini?” amehoji Lyamongi.
Amesema maswali hayo yanapaswa kuwa sehemu ya majadiliano ya wadau ili kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanaendelea kuwa na mchango wenye tija katika maendeleo ya Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla.
Kaimu Katibu Tawala huyo amesema maendeleo hayawezi kupatikana bila ubunifu, hivyo ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuacha kutegemea mifumo ya zamani ya utekelezaji wa miradi na badala yake kubuni njia mpya za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Amesema ubunifu unaweza kujumuisha matumizi ya teknolojia, kuboresha utoaji wa huduma, ukusanyaji na matumizi ya taarifa, uhamasishaji wa jamii, uzalishaji wa bidhaa na huduma, pamoja na kuanzisha ushirikiano katika kutafuta na kutumia rasilimali.
Aidha, ameyataka mashirika hayo kuwekeza zaidi katika teknolojia na uchumi wa kidijitali, akieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, mawasiliano, ukusanyaji wa taarifa, uhamasishaji wa jamii na kutafuta fursa za kifedha.
Lyamongi pia ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali zinazoendana na malengo yao ya kijamii, hatua ambayo inaweza kuongeza uwezo wa taasisi kujigharamia na kupunguza utegemezi wa wafadhili.
Lyamongi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayotekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na mipango ya maendeleo ya Serikali.
Amesema Serikali inataka kuona miradi inayotekelezwa na mashirika hayo ikiendana na mahitaji halisi ya wananchi na vipaumbele vya Serikali, huku ikiweka msingi wa maendeleo endelevu katika jamii.
“Tusiwe na miradi inayokuja na kuondoka bila kuacha uwezeshaji wa kudumu katika jamii. Tunatamani kuona miradi inayojenga uwezo wa wananchi kujitegemea,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inakaribisha ushirikiano na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo utekelezaji wake umeanza rasmi mwezi Julai mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Lyamongi amewataka washirika wa maendeleo na wafadhili kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwekeza kwenye miradi yenye tija na inayojenga uwezo wa wananchi.
Amesema ni muhimu kuhamia kwenye miradi inayowezesha jamii kujitegemea badala ya miradi inayowafanya wananchi na taasisi kuwa na utegemezi wa kudumu wa ufadhili.
Lyamongi amesisitiza umuhimu wa utawala bora, uwajibikaji, ushirikiano na matumizi sahihi ya rasilimali, akisema kila shirika linapaswa kuwa na mifumo madhubuti ya kusimamia fedha na kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya jamii.
Amesema kaulimbiu ya kongamano hilo inapaswa kuwa ukumbusho kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine kwamba:
“Uendelevu hauanzi na fedha nyingi; unaanza na fikra sahihi, ubunifu, ushirikiano na matumizi bora ya rasilimali zilizopo.”













































