` CCM NA ACT-WAZALENDO ZASISITIZA UMUHIMU WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR KWA USTAWI WA MUUNGANO

WANDAMAN HOTEL

CCM NA ACT-WAZALENDO ZASISITIZA UMUHIMU WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR KWA USTAWI WA MUUNGANO


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ni muhimu kwa ustawi wa Tanzania, huku kikieleza kuwa mfumo huo unatoa uhakika wa utulivu unaonufaisha Jamhuri ya Muungano mzima kwa kuwa Zanzibar ni sehemu isiyotenganishwa ya muungano huo.
Msimamo huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, wakati akizungumza katika siku ya pili ya mkutano wa kitaifa wa wadau ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwa ajili ya kutafakari hali ya siasa nchini.

Wasira alisisitiza kuwa amani na utulivu wa pande zote mbili unategemeana tangu mwaka 1964 hadi leo, akifafanua kuwa changamoto za upande mmoja huathiri moja kwa moja upande wa pili hasa ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya Wazanzibari wanaoishi Bara ni moja ya matunda chanya ya Muungano huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, alithibitisha utayari wa chama chao kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kueleza kuwa tayari wamewasilisha mapendekezo kuhusu mambo saba ya msingi.

Othman, ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika serikali hiyo, alieleza kuwa wanatambua vyema umuhimu wake katika kujenga mustakabali wa taifa kwa kuwa walishiriki kuipambania, akiongeza kuwa nia yao kuu ni kushirikiana na wenzao kujenga nchi kwa manufaa ya wananchi wote badala ya kususia.

Alitoa shukrani za pekee kwa viongozi wastaafu wa CCM kwa kuonyesha busara na mchango mkubwa uliowezesha kufikia upatanisho uliopo sasa.

Akiashiria mchakato wa mazungumzo ya kisiasa, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismael Jussa Ladhu, alieleza kuwa mafanikio ya maridhiano hayahitaji kila wakati kusimamiwa na watu kutoka nje, akisisitiza kuwa viongozi wanapokaa wenyewe na kuzungumza kwa uwazi huku wakisomana mioyo yao, wanaweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464