
MAAFISA MAENDELEO SHYDC WAFANYA USAFI WA
MAZINGIRA WATOA MSAADA KITUO CHA AFYA NINDO
Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
Umoja wa Maafisa Maendeleo wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, umeendelea na zoezi la usafi pamoja na kugawa mahitaji mbalimbali kwa wazazi katika Kituo cha Afya Nindo, ikiwa ni sehemu ya kilele cha Mwezi wa Maafisa Maendeleo ndani ya halmashauri hiyo.
TAZAMA VIDEO👇👇
Zoezi hilo la limefanyika leo Septemba
29,2026 ambapo jana walikuwa katika kituo cha Afya cha Tinde.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Kitengo
cha Divisheni ya Utumishi wa Umma, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata ya
Mwalukwa Elpendo John, amesema hatua hiyo inalenga kuwa mfano hai wa kuigwa na
jamii, huku akiwataka wananchi kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao, ili
kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño
zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba.
Sambamba na hilo, Afisa Afya wa Kituo
cha Afya Nindo, Jibril Adam, kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,
amepongeza Umoja huo chini ya Mkuu wa Kitengo cha Divisheni ya Utumishi wa Umma
wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa msaada walioutoa, pamoja na
kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia zoezi la usafi.
Amesema Umoja huo ni mfano wa kuigwa na
taasisi mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Mkoa wa
Shinyanga kwa ujumla.
Aidha, Afisa huyo amesema msaada
uliotolewa kwa wazazi katika kituo hicho utawasaidia kutekeleza majukumu ya
malezi na matunzo ya watoto, kwa kuwa baadhi ya wazazi hushindwa kumudu gharama
za mahitaji kutokana na hali duni ya maisha.
Nao baadhi ya wazazi katika kituo hicho, akiwemo Getruda Juma na Elizabeth Mathias, wameeleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa na Umoja huo, wakisema msaada huo utawasaidia wazazi ambao wakati mwingine hushindwa kumudu gharama za mahitaji mbalimbali pindi wanapojifungua.
























