` WASIRA ATAKA MAKUNDI YOTE TUME YA MARIDHIANO

WANDAMAN HOTEL

WASIRA ATAKA MAKUNDI YOTE TUME YA MARIDHIANO


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ni muhimu kwa tume itakayoundwa kwa ajili ya mchakato wa maridhiano ishirikishe makundi yote ili kupata mwafaka wa kitaifa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira alisema hayo alipozungumza na Kituo cha televisheni cha UTV cha Kampuni ya Azam Media ya Dar es Salaam juzi.

“Maridhiano ya kweli ni kuwaleta Watanzania katika makundi mbalimbali pamoja..Tume lazima ishirikishe makundi, yote kosa linalofanyika ni kuwa Chadema wanadhani tunataka kuridhiana na wao,” alisema Wasira.
Alisema si sahihi kutumia maridhiano kama kigezo cha kuvunja sheria na kuwa maridhiano yasitumiwe kuvunja sheria bali yatumike kuwaunganisha wananchi.

“Yapo maridhiano lakini kwa sheria na si vizuri nchi yetu ikajenga taswira kwamba ukikosea sheria basi jibu lake litakuwa maridhiano,” alisema Wasira.

Kuhusu uchaguzi ndani ya CCM alisema chama hicho kinakusudia kuzingatia kanuni za kuchagua viongozi ikiwemo viongozi watakaochaguliwa kuwa na uwezo katika nafasi wanazoomba pamoja na kuwa na misimamo isiyoyumba na kufanya maamuzi.

Pia, Wasira alionya wanaoanza kujitokeza na kutengeneza makundi kuwania nafasi za uongozi akisema vitendo hivyo ni uvunjaji wa kanuni za uchaguzi ndani ya chama.

“Katika uchaguzi unaokuja tunakusudia kuzingatia kanuni kiongozi atakayependekezwa kuchaguliwa tunataka awe na msimamo usioyumba na uwezo wa nafasi anayoomba... Sisi tunajua vyeo vyote kuna watu wanakuwa na nia lakini tunazuia ujengaji wa safu huwezi kujitokeza utuambie wewe unataka urais sasa hivi,” alisema.

Akizungumzia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya 2025 alisema imetekelezwa kwa kiwango cha juu kwa kukamilisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kituo cha Kuzalisha umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) na kwa sasa utekelezaji wa ilani ya 2030 unaendelea ikiwemo mchakato wa kupata katiba mpya akisisitiza kuwa mchakato wa kupata katiba mpya hauwezi kucheleweshwa na maridhiano. Wasira alihimiza Watanzania walinde amani na utulivu ili nchi itimize malengo ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi.






Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464