Ushindi huo wa kihistoria ulitangazwa wakati wa hafla ya 33 ya World Travel Awards iliyofanyika Agosti 28, 2026 katika Hoteli ya Diamonds Bijoux, Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar, na kuifanya TAWA kuanza safari yake katika tuzo hizo kwa mafanikio makubwa baada ya kuingiza maeneo matatu katika kategori mbalimbali na mawili kati yake kuibuka washindi. Maeneo hayo ni Hifadhi ya Selous, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere pamoja na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo yaliingia katika ushindani dhidi ya baadhi ya vivutio vinavyotambulika zaidi katika sekta ya utalii barani Afrika.
Katika kategori ya Africa's Leading Tourist Attraction 2026, Selous, Mpanga-Kipengere na Kilwa Kisiwani zilichuana na baadhi ya vivutio maarufu zaidi barani Afrika vikiwemo Pyramids of Giza nchini Misri, Table Mountain, Robben Island na V&A Waterfront nchini Afrika Kusini, Okavango Delta nchini Botswana na Lake Malawi, huku ushindani kutoka Tanzania ukihusisha pia Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Misitu ya Asili ya Amani na Hifadhi ya Msitu wa Pugu Hills, ambapo katika ushindani huo mkubwa Hifadhi ya Selous iliibuka mshindi na kuweka historia kwa TAWA katika ushiriki wake wa kwanza.
Kwa upande wake, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere nayo iliandika historia baada ya kuibuka mshindi katika kategori ya Africa's Leading Honeymoon Destination 2026 ikichuana na Marrakech nchini Morocco, Visiwa vya Msumbiji, Okavango Delta nchini Botswana, Red Sea Riviera nchini Misri, Hifadhi ya Taifa ya Volcanoes nchini Rwanda pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, aliwashukuru Watanzania kwa kuvipigia kura vivutio hivyo na kuchangia ushindi huo huku akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ubunifu, bidii na kujituma kwa Bodi, Menejimenti na watumishi wa TAWA katika kuhakikisha maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka yanaendelea kuboreshwa na kuwa na mvuto zaidi kwa shughuli za utalii, akisisitiza kuwa ushindi huo unaongeza nguvu katika dhamira ya TAWA ya kuendeleza utalii wa ndani na kufungua zaidi maeneo hayo kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.
Naye Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, mbali na kuwapongeza Watanzania waliovipigia kura vivutio hivyo, alisema Selous na Mpanga-Kipengere ni sehemu tu ya hazina kubwa ya vivutio vinavyosimamiwa na Mamlaka katika maeneo mbalimbali nchini, huku akibainisha kuwa TAWA inaendelea kuboresha miundombinu ili kuongeza mvuto na kuziwezesha huduma kufikiwa kwa urahisi zaidi na wageni.
Ushindi huo wa Selous na Mpanga-Kipengere unaifanya Agosti 28, 2026 kuwa siku muhimu katika historia ya TAWA, huku ukidhihirisha uwezo wa maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka kushindana na vivutio vyenye majina makubwa katika soko la utalii la Afrika na kimataifa, jambo linaloongeza mwonekano wa hazina ya vivutio vya Taifa, kufungua fursa zaidi za kuitangaza Tanzania na kuonyesha utofauti wa bidhaa za utalii kuanzia wanyamapori na mandhari ya asili hadi urithi wa kihistoria na kiutamaduni ikiwa ni mwaliko mwingine kwa dunia kuja kuigundua Tanzania.

