Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana nchini wanaendelea kunufaika na fursa za nje ya nchi na zenye staha kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Agosti 27,2026 wakati wa uzinduzi wa mkopo wa Ughaibuni Loan unaoratibiwa na Benki ya CRDB pamoja na kuwaaga vijana 130 kati ya 530 wanaotarajia kwenda kufanya kazi nje ya nchi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi amesema Serikali inatambua ajira za nje ya nchi kama nyenzo muhimu ya kupanua fursa za ajira, kuongeza kipato cha vijana, kukuza ujuzi na kuwajengea uzoefu wa kimataifa.
“Matokeo ya jitihada hizi yamewezesha Watanzania 14,613 kupata ajira nje ya nchi tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani. Kati ya Julai 2025 hadi sasa, Watanzania 8,428 wameunganishwa na waajiri nje ya nchi,” amesema Dkt. Munisi.
Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuendelea kuaminika kuwa na nguvu kazi salama na yenye staha duniani.
Kuhusu uzinduzi wa Ughaibuni Loan, Dkt. Munisi amesema mkopo huo unalenga kuwawezesha vijana waliopata ajira nje ya nchi kupata fedha nafuu za kugharamia maandalizi ya safari ikiwemo tiketi ya ndege, bima na visa.
“Ughaibuni Loan siyo msaada bali ni mkopo wa uwezeshaji. Nawasihi vijana wahakikishe wanafanya marejesho ili na wengine wapate fursa,” amesisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Bw. Pendason Philemon amesema benki imetenga jumla ya Shilingi bilioni 250 kwa miaka mitano kutoa mikopo ya kati ya Sh. 500,000 hadi milioni 20 kwa kila kijana kulingana na gharama za kufika kwa mwajiri wake.
“Kigezo muhimu ni kuwa na mkataba au barua ya ajira iliyothibitishwa na wakala. Marejesho yatakuwa kwa miezi 24 na tunatoa kipindi cha neema cha miezi 2 kwa riba ya asilimia 15,” amesema Philemon.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Binafsi wa Ajira TRAA, Bw. Abdala Khalid amesema mkopo huo utawaepusha vijana na watu wasio na nia njema.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Zuhura Yunus amesema Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi,Ajira na Mahusiano inaendelea kutafuta masoko ya uhakika ya ajira ikiwemo Saudi Arabia, Oman, Qatar, Denmark na Ujerumani.
Mmoja wa wanufaika, Dickson Tadeo Mbaga amesema kupitia mkopo huo aliweza kugharamia visa, tiketi na bima. “Ninawasihi vijana wenzangu wachangamkie fursa hii,” amesema.
Serikali imesema itaendelea kuhakikisha vijana 530 wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni katika fani mbalimbali ikiwemo ujenzi wanalindwa na kazi zao zinakuwa zenye staha.
