` NDEJEMBI AAPISHWA! RAIS SAMIA AMWAMBIA 'CHEO SI UFALME, NI DHAMANA'

WANDAMAN HOTEL

NDEJEMBI AAPISHWA! RAIS SAMIA AMWAMBIA 'CHEO SI UFALME, NI DHAMANA'


 Nafasi ya Makamu wa Rais inahitaji uongozi wenye kuunganisha watu, kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali na kutanguliza maslahi ya Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,baada ya kushuhudia uapisho wa Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais,Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

“Cheo si ufalme, ni dhamana. Dhamana uliyopewa ni ya kuwatumikia Watanzania,” amesema Rais Dkt. Samia,akimuasa kutekeleza dhamana hiyo kwa uzalendo, bidii, uadilifu na uwajibikaji.

Akizungumza katika hafla ya uapisho Agosti 29 , 2026, Ikulu Chamwino, mkoani Dodoma, Rais Dkt. Samia amesema uzoefu wa Mheshimiwa Ndejembi katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika Serikalini, pamoja na bidii, uwezo wa kujifunza, kufuatilia na kusimamia vyema dhamana anazopewa, unampa msingi mzuri wa kutekeleza wajibu wake mpya katika nafasi ya Makamu wa Rais.

Aidha, amemtaka Makamu wa Rais kuendelea kuimarisha umoja, mshikamano, ushirikiano na utulivu, huku akishirikiana na viongozi wengine katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Ameongeza kuwa, matarajio ya wananchi kuhusu maendeleo yanaweza kufikiwa kwa Serikali na viongozi wake kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu na uongozi bora katika kila ngazi.

Rais Dkt. Samia amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji uongozi unaosukuma matokeo na kutanguliza maslahi ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameipongeza Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi kwa kuridhia jina la Mheshimiwa Ndejembi, akisema uteuzi wake umezingatia uwezo, uzoefu na sifa za kiuongozi.

Amesema umri wa Mheshimiwa Ndejembi unampa nafasi ya kutumia nguvu na maarifa yake katika kulitumikia Taifa, huku akimtaka kuendelea kujifunza na kukua katika majukumu yake mapya.

Mheshimiwa Ndejembi ameapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi, na baadaye uteuzi wake kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
































Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464