Dar es Salaam — Shekh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Sheikh Hemed Jalala, amewataka Watanzania kuenzi mafundisho ya Mtume Muhammad (Swallallahu Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) kwa kudumisha ukweli, uaminifu, kuvumiliana, upendo, amani na mshikamano, akisema maadili hayo ni muhimu katika kurejesha mshikamano wa kitaifa.
Sheikh Jalala ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, akisisitiza kuwa mafundisho ya Mtume yanapaswa kuwa msingi wa kujenga jamii yenye maadili na kuheshimiana licha ya tofauti za dini, madhehebu, mitazamo na fikra.
Akinukuu Qur’ani, Sheikh Jalala amesema Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume Muhammad kwa kusema “Wa innaka la'ala khuluqin 'adheem”, akieleza kuwa Mtume alikuwa na tabia na maadili mema ya kuigwa na jamii.
Amesema miongoni mwa mafunzo makubwa ya Mtume ni ukweli na uaminifu, akisisitiza kuwa misingi hiyo inahitajika katika kipindi ambacho jamii inakabiliwa na changamoto za kimaadili.
“Moja ya jambo la kulisoma katika masomo ya Mtume Muhammad na katika mwenendo wake ni watu kuwa wakweli katika kazi zao, shughuli zao, kuwajibika kwao na kusimamia kila jambo,” amesema.
Aidha, Sheikh Jalala amesisitiza umuhimu wa kuvumiliana na kuheshimu watu wenye mitazamo tofauti, akieleza kuwa Mtume Muhammad aliishi na jamii zenye tofauti za kidini na kimtazamo huku akijulikana kwa ukweli na uaminifu.
Amesema Tanzania inahitaji kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu, akitaja umuhimu wa Waislamu wa madhehebu mbalimbali, wakiwemo Shia na Sunni, kutambua kuwa wote ni Waislamu na wanapaswa kushirikiana.
“Leo kama kuna jambo ambalo Tanzania inalihitaji ni sisi Watanzania, Waislamu, Wakristo, Mayahudi, Wapagani na wenye dini tofauti kuwa na umoja wetu na kutambua kwamba sisi sote ni wanadamu na sote ni Watanzania,” amesema.
Sheikh Jalala pia ametoa wito wa kulinda amani, upendo, mshikamano na maridhiano nchini, akisema maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume yanapaswa kuwa kichocheo cha Watanzania kuwa kitu kimoja.
Ameomba Mwenyezi Mungu aendelee kuilinda Tanzania na kuwapa viongozi nguvu katika kuhakikisha wananchi wanadumisha mshikamano, upendo na amani.
WADAU WOTE WAHITAJIKA KUREJESHA MAADILI
Akijibu swali kuhusu namna ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana, Sheikh Jalala amesema jukumu hilo haliwezi kubebwa na kiongozi mmoja au kundi moja pekee, bali linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Ametaja wazazi, viongozi wa dini, mamlaka za Serikali pamoja na vyombo vya habari na mitandao kuwa miongoni mwa wadau muhimu katika kujenga maadili ya vijana na jamii kwa ujumla.
Amesema hakuna sababu ya kulaumu viongozi wa dini pekee kutokana na changamoto za maadili, kwa kuwa kila mdau ana wajibu wa kushiriki katika malezi na ujenzi wa jamii yenye maadili.
MATEMBEZI YA ZIFA YAENDELEZA UJUMBE WA UPENDO
Kwa upande wake, Sheikh Maulid Rume kutoka taasisi ya Sayyid Shuhadaa Al-Aalamiyyah, amesema matembezi ya Zafa yaliyofanyika katika maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha furaha, upendo, mshikamano, uzalendo na utu.
Amesema matembezi hayo yanafanyika kwa lengo la kuenzi kuzaliwa kwa Mtume Muhammad na kueneza furaha katika jamii, akisisitiza kuwa mafundisho ya Mtume yanapaswa kuonekana kupitia matendo yenye kuleta huruma na mshikamano.
Sheikh Rume amesema kuingiza furaha katika moyo wa mwanadamu ni miongoni mwa mambo muhimu katika mafundisho ya Kiislamu, hivyo waumini wanapaswa kuhakikisha ibada na matendo yao yanaambatana na kuwajali na kuwafurahisha wengine.
Amesema maadhimisho hayo, yanayofanyika tarehe 17 ya Mfungo Sita kwa mujibu wa wafuasi wa Ahlul Bayt, ni sehemu ya kuendeleza ujumbe wa Mtume wa kuondoa huzuni, kuleta furaha, huruma na mshikamano miongoni mwa wanadamu.
“Ni lazima tuyadumishe haya kwa sababu haya hayatapatikana nje ya Mtume wetu Muhammad,” amesema.
Sheikh Rume amewataka Watanzania kuendelea kulinda umoja na amani ya nchi, akisema Tanzania inapaswa kubaki kuwa taifa lenye furaha, mshikamano na upendo.
Amesema maadhimisho hayo yataendelea kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo sherehe ya Maulidi iliyopangwa kufanyika baadaye katika siku hiyo.








