
MWENGE WARIDHISHWA NA UKARABATI WA MADARASA SHULE YA SEKONDARI OLD SHINYANGA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mwenge wa Uhuru umekagua na kuridhishwa na ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa katika shule ya Sekondari Old Shinyanga, uliogharimu Shilingi milioni 58, fedha kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Serikali Kuu.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Wazo Mwang’onda, akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, amesema ukarabati huo ni maandalizi ya kupokea wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza mwaka 2027, ambapo madarasa mawili yatakayokamilika yatatumika kupokea wanafunzi hao.
Aidha, ameipongeza Manispaa ya Shinyanga kwa kufanya ukarabati huo, ambao utawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia, huku akitoa ushauri kwa Manispaa hiyo, kuendelea kujenga madarasa mengine mapya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mwenge wa Uhuru ukiwa shuleni hapo, umezindua Klabu ya Wapinga Rushwa, huku wanafunzi wakitakiwa kusambaza elimu ya kupinga rushwa ndani ya jamii.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464


