EACOP YAACHA URITHI WA UJUZI: WATANZANIA ZAIDI YA 100 WAANDALIWA KUENDESHA MRADI
Na Neema Nkumbi, Masumbwe Geita
Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) umeanza kuacha urithi wa ujuzi kwa Watanzania, huku zaidi ya 100 kati yao wakipatiwa mafunzo maalumu ya kuwa sehemu ya timu itakayoendesha mradi huo baada ya kukamilika.
Hatua hiyo imekuja wakati utekelezaji wa mradi ukiwa umefikia hatua za mwisho, huku ujenzi wa Kituo cha Nne cha Kusukuma Mafuta (PS4) ukifikia karibu asilimia 90 na mradi mzima upande wa Tanzania ukitarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Desemba 2026.
Msimamizi wa Local Content katika EACOP, Neema Kweka, amesema mkakati wa mradi haujaishia katika kutoa ajira kwa Watanzania, bali umejikita pia katika kuhakikisha ujuzi unaopatikana kupitia mradi huo unabaki nchini na kutumika katika miradi mingine.
Amesema utekelezaji wa Local Content umejikita katika maeneo manne, ambayo ni ajira kwa Watanzania, kuwajengea ujuzi, kuhakikisha manunuzi yanafanyika ndani ya Tanzania na kujenga uwezo wa kampuni za wazawa.
“Kwanza Watanzania wananufaika na ajira kwenye mradi, lakini jambo la pili ni kuhakikisha kwamba wanapata ujuzi, na jambo la tatu ni kuhakikisha kwamba manunuzi ya muhimu ya mradi kwa watoa huduma wetu wa ndani yanaweza kununuliwa ndani ya nchi yetu,” amesema Kweka.
Amesema zaidi ya Watanzania 100 tayari wamepatiwa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kushiriki katika uendeshaji wa mradi baada ya awamu ya ujenzi kukamilika.
“Mradi utakapofika mwisho, Watanzania ambao wametengewa ujuzi wa kipekee ndio wataendesha operesheni ya mradi huu,” amesema.
AJIRA ZAWAFIKIA WATANZANIA 909 PS4
Ujenzi wa PS4 pia umeibua fursa kubwa za ajira kwa Watanzania.
Mkurugenzi wa Masuala ya Watu wa EACOP na Kaimu Meneja wa EACOP Tanzania, Geofrey Mpoda, amesema kati ya wafanyakazi 1,121 waliopo katika eneo hilo, Watanzania ni 909.
“Jumla ya wafanyakazi waliopo hapa wanaofanya kazi ni 1,121. Kati ya hao, 909 ni Watanzania,” amesema Mpoda.
Amesema ajira hizo zimehusisha watu wenye viwango tofauti vya ujuzi, kuanzia wataalamu wenye ujuzi maalumu, wenye ujuzi wa kati hadi wasio na ujuzi maalumu.
Kwa mujibu wake, katika maeneo mbalimbali ya mradi zaidi ya asilimia 80 ya ajira zimetolewa kwa wazawa, huku wataalamu wa kigeni wakitumika zaidi katika maeneo yenye ujuzi maalumu ambao bado haujapatikana kwa kiwango cha kutosha nchini.
“TULIANZA KAMA WASAIDIZI, SASA TUMEKUWA MAFUNDI”
Mabadiliko hayo yanaonekana pia kwa baadhi ya Watanzania walioshiriki katika ujenzi wa EACOP.
Paulo Chasama Cosma, mzawa wa Mbeo, amesema alijiunga na mradi huo mwaka 2024 akiwa msaidizi wa fundi, lakini kupitia mafunzo na uzoefu alioupata kazini amepanda hadi kuwa fundi mwenye uwezo wa kufanya kazi mbalimbali za kiufundi.
“Nimeingia kama saidia fundi. Imeniwezesha kupata maarifa mengi na uelewa wa jinsi ya kufanya kazi kwa upana. Lakini sasa nipo kama fundi, naweza kushika mashine ya welding, kukata na kufanya maeneo mbalimbali,” amesema Paulo.
Amesema ajira hiyo imemsaidia kupata kipato cha kugharamia mahitaji ya familia yake, ikiwemo chakula na mahitaji ya watoto.
Naye Ismail, mkazi wa Uungaji, amesema mradi huo umewapa wananchi fursa ya kujiingiza katika sekta mbalimbali na kupata kipato cha kuendesha familia zao.
“Mradi huu umetunufaisha kwa kiasi kikubwa sana. Umetuwezesha kujiingiza katika sekta mbalimbali. Katika sekta mbalimbali unaweza kupata kipato cha kuendesha familia yako,” amesema Ismail.
VETA NA SIDO WAINGIA KATIKA KUJENGA UWEZO
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa TPDC, Derick Moshi, amesema Serikali kupitia TPDC imekuwa ikishirikiana na VETA na SIDO katika kuwaandaa vijana kupata ujuzi unaohitajika katika sekta za mafuta, gesi, viwanda na uhandisi.
Amesema vijana wanaopata mafunzo hayo pia wanapata uzoefu wa moja kwa moja kupitia ajira kwenye miradi, hali inayowaongezea uwezo wa kushiriki katika miradi mingine mikubwa nchini.
“Pamoja na kwamba wanafundishwa, wanapata ajira na experience. Unaona kabisa kwamba Tanzania ya viwanda, Tanzania ya uchumi huu inakuja kule mbele,” amesema Moshi.
MIUNDOMBINU YA EACOP YAWEZA KUTUMIKA KWA MAFUTA YA TANZANIA
Mbali na ajira na ujuzi, TPDC inaona mradi huo kama sehemu ya maandalizi ya Tanzania kwa matumizi ya rasilimali zake za mafuta na gesi hapo baadaye.
Moshi amesema TPDC inaendelea na ukusanyaji, uchakataji na tafsiri ya data katika shughuli za utafutaji wa mafuta, huku akieleza matumaini ya Tanzania kugundua vyanzo vyake vya mafuta.
“Tunaamini kabisa kwamba baada ya muda mfupi sana tutatoka mbele na kutangaza, ‘yes, tumeweza kupata vyanzo vya mafuta.’ Hilo ndiyo ndoto zetu,” amesema.
Amesema endapo Tanzania itagundua mafuta yake, miundombinu inayojengwa kupitia EACOP inaweza kuwa na umuhimu katika kuyasafirisha na kuyafikisha kwenye masoko.
EACOP inaunganisha maeneo ya uzalishaji mafuta ya Kabaale-Hoima nchini Uganda na Chongoleani, Tanga, nchini Tanzania kupitia bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1,443.
Hivyo, wakati mradi ukiingia katika hatua zake za mwisho za ujenzi, wadau wanaeleza kuwa moja ya matokeo muhimu yanayoweza kubaki nchini ni nguvu kazi yenye ujuzi, kampuni zenye uwezo na uzoefu wa kutekeleza miradi mikubwa ya mafuta, gesi na miundombinu.



























