` MAKONDA ATAKA SALUNI KUHUBIRI AMANI

WANDAMAN HOTEL

MAKONDA ATAKA SALUNI KUHUBIRI AMANI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wamiliki na wafanyakazi wa saluni nchini kote kumtanguliza Mungu katika shughuli zao na kugeuza maeneo hayo kuwa vituo vya kuhubiri amani, huku akitoa onyo kali dhidi ya wimbi la chuki na uchochezi wa vurugu unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. 

Makonda amesema kuwa katika ulimwengu wa sasa ambapo mitandao ya kijamii inajazwa na habari za kuvunja moyo na mikanganyiko, kuna haja kubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla kutafuta amani ya kweli inayotokana na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Amesema kuwa tangu alipopewa dhamana ya uongozi amekuwa akimtanguliza Mungu katika kila hatua, jambo ambalo limekuwa siri ya kufunguka kwa milango ya mafanikio yake.

Waziri huyo amewahimiza wafanyakazi wa saluni kutochoka kumwomba Mungu na kuhakikisha kuwa wanailinda amani ya nchi na ya mioyo yao, kwani mafanikio ya kweli yanatokana na utulivu na baraka katika kazi za mikono yao na si katika kufuata kelele au vurugu zinazochochewa mtandaoni.

Aidha, amesisitiza kuwa ni muhimu saluni ziwe maeneo salama yanayofariji na kuleta utulivu, ili kuruhusu watu kufanya kazi zao kwa uhuru na kujipatia kipato cha halali. 

Makonda amebainisha kuwa vijana wengi wamekuwa wakipoteza amani zao kwa sababu ya kutamani au kuiga maisha ya bandia wanayoyaona kwenye mitandao ya kijamii, bila kujua changamoto na maumivu wanayoyapitia watu hao nyuma ya pazia. 

Amesema kuwa wakati mwingine mtu anaweza kuonekana ana maisha mazuri mtandaoni lakini kumbe ndani ya moyo wake anatamani utulivu na amani aliyonayo mtu wa kawaida. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464