` WATUHUMIWA 130 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUPANGA NA KUHAMASISHA UCHOCHEZI

WANDAMAN HOTEL

WATUHUMIWA 130 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUPANGA NA KUHAMASISHA UCHOCHEZI



Jeshi la Polisi Tanzania limefanikiwa kuwatia mbaroni jumla ya watuhumiwa 130 katika mikoa mbalimbali nchini ambao walikuwa wanapanga, kushiriki katika vikao vya ndani, na kuandaa pamoja na kusambaza taarifa za uchochezi ili kuhamasisha vitendo vya kihalifu visivyokubalika.
Hatua hii inafuatia ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na jeshi hilo dhidi ya uhalifu uliokuwa unahamasishwa na wahalifu hao kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ikiwemo vikao vya ndani. Kwa sasa, uchunguzi dhidi yao unakamilishwa ili hatua zingine za kisheria ziweze kufuata.
Ukamataji huo umetokana na kubainika kwa mipango na matamko ya kihalifu yaliyolenga kuhamasisha watu kushiriki katika vitendo vya uvunjifu wa amani. 
Miongoni mwa vitendo hivyo ni pamoja na mipango ya kuua baadhi ya viongozi na wananchi, kuchoma moto shule, kulipua transforma za umeme ili kuingiza nchi kwenye giza, kuharibu na kupora mali za umma na za watu binafsi, pamoja na kuua askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha zao.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama limewatoa hofu wananchi na kueleza kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, na kwamba linaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha usalama unaendelea kuwepo ili wananchi waendelee na shughuli zao za kujitafutia riziki katika mazingira ya amani na utulivu. 
Aidha, jeshi hilo linaendelea kuwafuatilia kwa karibu watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa ili nao wafikishwe mbele ya sheria.
Kamanda Misime ametoa wito kwa jamii kwamba endapo mtu yeyote atatumiwa ujumbe unaohamasisha vitendo vya kihalifu kupitia mitandao, asiusambaze bali aufute mara moja. 
Pia amewataka wananchi wote kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka kushiriki katika kuandaa na kusambaza taarifa zenye kuhamasisha vitendo vya kihalifu au kusambaza taarifa ambazo hazina uhakika na hawajui chanzo chake.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464