` WAKULIMA WA KOROSHO WAMSHUKURU RAIS SAMIA

WANDAMAN HOTEL

WAKULIMA WA KOROSHO WAMSHUKURU RAIS SAMIA

  

Na Mwandishi Wetu

Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha wanapata pembejeo za kilimo kwa wakati, hatua ambayo wamesema itawawezesha kujiandaa mapema kwa msimu wa uzalishaji.

Wakulima hao wameanza kupokea pembejeo mbalimbali ikiwemo dawa za maji na dawa ya unga (Sulphur), huku wakieleza kuwa upatikanaji wake kwa wakati ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuboresha sekta ya kilimo.

Mkulima wa korosho kutoka kijiji cha Nansinji, Rashid Hamid maarufu kwa jina la Mkapa, alisema wakulima wanathamini juhudi za Rais Samia za kuhakikisha pembejeo zinapatikana licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia.

"Sisi wakulima tunatambua jitihada za Rais Samia kutupatia pembejeo. Hatukutarajia kupata kwa urahisi kutokana na changamoto za upatikanaji wa bidhaa duniani zilizotokana na migogoro mbalimbali. Kupatikana kwa dawa hizi ni jambo la kutia moyo na linaonyesha namna Rais anavyowathamini na kuwapambania wakulima," alisema.

Kauli hiyo ilitolewa wakati wa ziara ya Afisa Tarafa, Emmanuel Shilatu, aliyefanya ukaguzi wa mwenendo wa ugawaji wa pembejeo ili kujiridhisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Shilatu alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imeendelea kuweka mazingira bora ya kuinua sekta ya kilimo kupitia utoaji wa pembejeo, mbegu bora, wataalamu wa ugani pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

"Kwa niaba ya wananchi, naungana nao kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa namna anavyowajali wakulima. Serikali imeendelea kuwapatia pembejeo, mbegu bora, wataalamu wa kilimo na kusimamia upatikanaji wa masoko ya mazao. Mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya kilimo hayawezi kutenganishwa na juhudi za Rais Samia," alisema Shilatu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kivukoni, Jackson Joseph Milanzi, aliishukuru Serikali kwa kupeleka pembejeo hizo na kuahidi kuhakikisha zoezi la ugawaji linaendelea kusimamiwa kwa uwazi, haki na usawa ili walengwa wote wanufaike.

Wakulima wa korosho nchini wameanza kupokea pembejeo mapema zaidi msimu huu ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo linalotarajiwa kuongeza uzalishaji, kuinua tija na kuboresha kipato cha wakulima.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464