Na Marco Maduhu, KSHAPU
Tamasha la utamaduni la Sanjo ya Busiya ambalo limefanyika katika Kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, limetoa wito kwa wananchi kuendeleza utamaduni, mila na desturi zao, pamoja na kudumisha upendo na amani ya nchi.
TAZAMA VIDEO👇👇
Ujumbe huo umetolewa leo Julai 7,2026 na Chifu wa Tatu wa Sanjo hiyo Chifu Faustine Makwai, wakati akizungumza na wananchi na machifu kutoka ndani na nje ya nchi waliohudhuria kwenye tamasha hilo.
Amesema, tamasha hilo la Sanjo ya Busiya ni la kumi na sita, ni nyenzo muhimu ya utamaduni kwa wana-Busiya na wananchi wa ujumla, ambalo linasisitiza upendo na kuwa wamoja.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mboni Mhita, amelipongeza tamasha hilo la utamaduni ambalo limekuwa likiwaunganisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali kusherehekea kwa pamoja siku ya Sabasaba na kuonyesha Tanzania ni nchi ya amani.
“Tamasha hili la utamaduni limeunganisha watu wengi na kuonyesha kuwa sisi ni damu moja na Watanzania wamoja. hivyo, tushirikiane katika kufanya kazi na kudumisha amani ya nchi yetu,” amesema Masindi.
Nao baadhi ya wananchi wa Kishapu, akiwamo Bugali Mbushi, wameeleza kuwa tamasha hilo limekuwa likiwajenga kuwa wamoja na kuendeleza mila na desturi zao.
Tamasha hilo limehudhuriwa na machifu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, zikiwamo nchi za Kenya na Afrika Kusini.
Chifu Faustine Makwaia wa tatu (Mwenyekofia ya Kitemi) akiongoza Tamasha la Sanjo ya Busiya wilayani Kishapu.