` SABASABA YADHIHIRISHA WANANCHI WANAJUA MSINGI WA AMANI NCHINI

WANDAMAN HOTEL

SABASABA YADHIHIRISHA WANANCHI WANAJUA MSINGI WA AMANI NCHINI


Kauli maarufu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitoa Desemba 9, 1961 kuhusu kuwasha Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro ili ulete tumaini, upendo, na heshima, inaendelea kuishi na kuonesha mwelekeo chanya katika mioyo ya Watanzania hadi sasa.
Katika maadhimisho ya kilele cha Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yaliyoenda sambamba na Siku ya Kiswahili Duniani mwaka 2026, imedhihirika kuwa mwangaza wa chombo hicho cha kitaifa umesaidia kuwazindua wananchi na kuwakumbusha umuhimu wa kulinda tunu ya amani kuliko kitu kingine chochote.

Ahadi hiyo ya kihistoria inazidi kudhihirika pale jamii inapokataa katakata kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha mustakabali na usalama wa nchi.

Uzoefu unaonesha kuwa Watanzania wamejifunza kutokana na makosa yaliyopita, hasa baada ya matukio yaliyojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika kipindi hicho, baadhi ya wananchi walijikuta wakiingizwa kwenye vurugu zilizosababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi, jambo ambalo liliacha majuto makubwa kwa walioshiriki kuandamana, kuunga mkono, au hata wale walioshindwa kutimiza wajibu wao wa kuzuia na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.

Somo hilo limekuwa darasa tosha kwa jamii kutambua kuwa vurugu hazina mshindi na kwamba ni vyema kuchagua heshima na amani kuliko kukimbilia mifarakano inayobomoa misingi ya nchi.

Kuelekea siku ya Sabasaba mwaka 2026, kuliibuka hamasa haramu kwenye mitandao ya kijamii zilizoratibiwa na watu waliopo ughaibuni wakishawishi kufanyika kwa maandamano yasiyokuwa na viongozi wala ajenda rasmi. Hata hivyo, kwa kutumia busara na kukumbuka ushauri wa viongozi wakuu wastaafu, Watanzania walichanganya akili zao na kuamua kutoshiriki kwenye mipango hiyo ya vurugu.

Badala yake, walitumia siku hiyo ya mapumziko kukaa na familia zao na wengine wengi walifurika kwenye Viwanja vya Sabasaba kujionea fursa za kibiashara na uwekezaji. Hatua hii imeonesha kuwa nchi imekomaa na wananchi wake wanathamini amani kama kiini cha maendeleo yote ya kiroho na kimwili, huku wakitambua kuwa rasilimali zote hazina thamani kama hakuna utulivu.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464