
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, amewaasa Maafisa Jenerali 17 waliostaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujiepusha na kujihusisha na masuala ya siasa, badala yake watulie na kuishi vizuri na familia zao katika maisha mapya ya uraiani.
Jenerali Mkunda alitoa kauli hiyo Julai 10, 2026, wakati wa hafla maalumu na ya kihistoria ya kuwaaga makamanda hao iliyofanyika katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Kikombo jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, CDF alifafanua kuwa ni ada na utamaduni wa jeshi kuwaaga watumishi wake kwa heshima kulingana na ngazi zao za utumishi, huku akibainisha kuwa baadhi ya majenerali hao wamelitumikia taifa hadi miaka 41.
Kwa mujibu wa kanuni za kijeshi bado maofisa hao wa ngazi za juu watakuwa katika hadhari ya mwito wa kijeshi kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo iwapo uhitaji utajitokeza.
Maafisa Jenerali 17 walioagwa katika hafla hiyo ya kipekee ni pamoja na Meja Jenerali Suleimani Mungiya Mzee, Meja Jenerali Paul Kisesa Simuli, Meja Jenerali Ramson Godwin Mwaisaka, Meja Jenerali Charles Peter Feruzi, na Meja Jenerali Julius Moses Gambos.
Upande wa Mabrigedia Jenerali walioagwa ni Brigedia Jenerali Mohamed Juma Mwakalikene, Brigedia Jenerali Omari Hamisi Majini, Brigedia Jenerali Anina Jonas Mkinga, Brigedia Jenerali Masele Alfred Machanga, Brigedia Jenerali Anchila Steven Kagombola, Brigedia Jenerali Method Kamugisha Matunda, Brigedia Jenerali Selemani Bakari Gwaya, Brigedia Jenerali Wema Laini Senzia, Brigedia Jenerali Kamandaz Makanya Erassy, Brigedia Jenerali Stanley Nathaniel Mjelwa, Brigedia Jenerali Ismail Shajack Ismail, pamoja na Brigedia Jenerali Charles Emilio Mwanziva.
Sherehe hizo zilipambwa na taswira ya kipekee ya kimila ya kijeshi ambapo magari maalumu matatu yaliyowabeba wastaafu hao yalisukumwa kwa mikono na maafisa wanaobaki kazini, ikiwa ni ishara ya heshima ya juu kabisa ya kijeshi na kuashiria mwisho wa utumishi wao uliojaa ukakamavu.
Pia kulifanyika gwaride rasmi la heshima lililofuatwa na zoezi la makamanda hao kukabidhi vitambulisho vyao vya kazi kwa Jenerali Mkunda, na kisha wao kukabidhiwa vitambulisho vipya vya ustaafu pamoja na funguo za magari mapya kabisa aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili ya matumizi yao.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa shamrashamra na tabasamu huku majenerali hao wakipiga picha ya pamoja ya kumbukumbu na Mkuu wa Majeshi, wakiondoka Kikombo Dodoma kwa heshima na vigelegele kuelekea maisha mapya ya kuitumikia jamii kwa namna nyingine.




