Diwani wa Kata ya Nyamalogo, Mheshimiwa Titus Philip Kalemela akikabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa niaba ya wananchi wake kwa kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga Andrea Mitumba Julai 16, 2026
NA MWANDISHI WETU
Diwani wa Kata ya Nyamalogo, Mheshimiwa Titus Philip Kalemela, kupitia Mfuko wa Nyamalogo Foundation, ameendelea kuonyesha dhamira ya dhati ya kuinua sekta ya elimu kwa kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao.
Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za mfuko huo, Mheshimiwa Kalemela amesema kuwa katika kipindi cha Juni hadi Julai 2026, Nyamalogo Foundation imefanikisha miradi mbalimbali ya elimu iliyolenga kuwapa watoto na vijana fursa ya kuendelea na masomo, licha ya changamoto za kifedha zinazowakabili baadhi ya familia.
Ameeleza kuwa mfuko huo ulianzishwa kwa lengo la kuiwezesha jamii ya Nyamalogo, hususan katika sekta ya elimu, kupitia ushirikiano wa viongozi, wadau wa maendeleo na wananchi wenye nia njema kutoka ndani na nje ya kata.
Katika mafanikio yaliyopatikana, mfuko huo umemwezesha Jumanne Kabadi Kashinje kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2026 katika Shule ya Sekondari Isaka kwa kugharamia ada na mahitaji mengine yenye thamani ya Shilingi 749,400. Jumanne alipata Daraja la Kwanza katika mtihani wake wa Kidato cha Nne, lakini alikuwa katika hatari ya kushindwa kuendelea na masomo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ya familia yake.
Aidha, mfuko huo umemsaidia Erick Lufunga Nkuba kujiunga na Chuo cha Ualimu Songea DC mkoani Ruvuma kusomea Stashahada ya Ualimu wa Masomo ya Sayansi (Kemia na Hisabati), kwa kumpatia msaada wa Shilingi 200,000, hatua inayompa nafasi ya kutimiza ndoto zake za kuwa mwalimu.
Mbali na hilo, Nyamalogo Foundation imegharamia mahitaji mbalimbali ya wanafunzi 43 kutoka shule za msingi za Nyamalogo, Mwang'osha, Shatimba, Mishepo na Mwampangabule kwa jumla ya Shilingi 602,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wanafunzi hao wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Katika kuimarisha lishe shuleni, Mheshimiwa Kalemela pia ametoa magunia 10 ya mahindi kwa shule zote zilizopo katika Kata ya Nyamalogo ili kusaidia mpango wa chakula shuleni. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora bila kukumbwa na changamoto ya njaa, hasa katika kipindi ambacho baadhi ya wazazi wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa kuchangia chakula shuleni.
Sambamba na hilo, wakazi wa Kijiji cha Nyamalogo wameendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia madawati 30 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 2, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini darasani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Andrea Mitumba, amepongeza hatua zinazochukuliwa na uongozi wa Kata ya Nyamalogo chini ya Mheshimiwa Titus Philip Kalemela kwa kuipa elimu kipaumbele.
Amesema elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa, hivyo ni muhimu kwa jamii kuendelea kuwekeza katika elimu ili kujenga kizazi cha vijana wenye maarifa kitakachochangia maendeleo ya nchi, ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Nyamalogo Foundation kutawasaidia watoto wengi kutoka familia zenye kipato cha chini kupata fursa ya elimu.
Aidha, Andrea Mitumba ameunga mkono juhudi za mfuko huo kwa kutoa mchango wa Shilingi laki moja, akieleza kuwa lengo lake ni kuendelea kuwasaidia vijana kufikia ndoto zao kupitia elimu. Pia amewahimiza wanafunzi walionufaika kutumia fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yao.
Baadhi ya wanafunzi waliopokea msaada huo wameushukuru uongozi wa Kata ya Nyamalogo na Nyamalogo Foundation kwa kuwapa matumaini mapya ya kuendelea na elimu. Wamesema watajitahidi kufanya vizuri katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao na baadaye kuisaidia jamii.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Nyamalogo, Veronica Maganga, amesema wananchi wa kijiji hicho wamekuwa mstari wa mbele kuchangia mpango wa chakula shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma hiyo muhimu na kujifunza bila vikwazo.
Viongozi wa Nyamalogo Foundation wameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa wa viongozi, wadau wa maendeleo na wananchi wenye moyo wa kujitolea. Wametoa wito kwa wafanyabiashara, taasisi na wadau wengine kuendelea kuunga mkono mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wenye uwezo wa kufanya vizuri darasani lakini wanaokabiliwa na changamoto za kifedha waweze kufikia ndoto zao.
Kupitia juhudi hizo, Nyamalogo Foundation inaendelea kuwa mfano wa mshikamano wa kijamii na uwekezaji katika elimu, ikiamini kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla.
Diwani wa Kata ya Nyamalogo, Mheshimiwa Titus Philip Kalemela akikabidhi madawati 30 kwa niaba ya wananchi wake kwa kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga Andrea Mitumba Julai 16, 2026