
Katika hatua muhimu ya kuimarisha sekta ya habari mtandaoni, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Bw. Beda Msimbe, amefanya ziara katika Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) leo tarehe 16 Julai 2026, ambapo amewasilisha ombi rasmi la kutolewa kwa mafunzo maalum kwa wanachama wa mtandao huo.
Katika mazungumzo yake na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, Bw. Msimbe amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika kuwajengea uwezo mabloga ili wafanye kazi kwa weledi, jambo litakalosaidia taifa kwa kiasi kikubwa.
Mabloga nchini kwa sasa wana jukumu kubwa la kujaza ombwe la taarifa katika nafasi ya kidijitali (space), ambapo wamekuwa mstari wa mbele kutangaza fursa, miradi ya maendeleo, na kuelimisha jamii kuhusu masuala anuai ya kitaifa.
Kwa kuzingatia mwenendo wa algorithm za kidijitali nchini Tanzania, maudhui yanayozalishwa na mabloga yamekuwa yakichochea mwamko mpya wa kizalendo na ukuaji wa uchumi wa kidijitali. Hivyo, mafunzo haya yatakuwa chachu ya kuongeza ubora wa maudhui hayo ili yaendane na viwango vya kisheria na kitaaluma.
Wakili Kipangula amepokea ombi hilo kwa mikono miwili na kukubaliana na Bw. Msimbe kuwa ushirikiano huu ni muhimu. Bodi imeahidi kutoa mafunzo yatakayolenga Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya uandishi, na umuhimu wa ithibati ili kuhakikisha mabloga wanafanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464