Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MBUNGE wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, amewataka vijana wanaofanya kazi ya usafirishaji wa abiria kwa pikipiki (bodaboda) katika Kata ya Tinde wilayani Shinyanga, kutokubali kushawishiwa au kurubuniwa kuvuruga amani ya nchi.
TAZAMA VIDEO 👇👇
Badala yake, amewasihi kudumisha utulivu, kuipenda nchi yao, na kuendelea kuzingatia shughuli zao za kiuchumi ili kujipatia riziki.
Mbunge Azza alibainisha hayo jana wakati akifungua vituo vitatu vya bodaboda katika Kata ya Tinde, ambavyo amewawezesha vijana hao kwa kuvijengea mabanda, ili kupata maeneo salama ya kufanyia kazi zao na kujistiri na jua na mvua.
Amesema kuwa, amani iliyopo nchini inapaswa kulindwa kwa nguvu zote ili kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo, akibainisha kuwa pasipo amani hakuna maendeleo, na kwamba Watanzania hawana sehemu nyingine ya kukimbilia.
"Hatutaki Jimbo la Itwangi, Kata ya Tinde na vijiji vyote kukosekane amani. Amani yetu ndiyo msingi wa kila kitu," amesema Azza.
Aidha, mbunge huyo amewahidi vijana hao, kuratibu semina maalum kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji na namna ya kukuza mitaji yao.
Ameongeza kuwa, tayari amemwomba Waziri mwenye dhamana ya masuala ya vijana Joel Nanauka, kupanga ratiba ili afike kuzungumza nao na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali.
"Nimesikia malalamiko mengi kuwa mkienda kusajili vikundi kuna vikwazo mnavyokutana navyo, changamoto zenu nimezipata na niko tayari kuzisimamia ili kuhakikisha mnasajili vikundi vyenu bila vikwazo, hivyo basi, tukiwaita kwenye semina ya ujasiriamali jitokezeni kwa wingi." Amesisitiza Azza.
Naye kiongozi wa kituo cha Bodaboda cha Tinde Simon Petro, amemshukuru mbunge huyo kwa kuwajengea vibanda hivyo, akieleza kuwa sasa wanafanya kazi katika mazingira salama tofauti na awali ambapo walikuwa wakiteseka na changamoto za jua kali na mvua.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa, amepongeza hatua hiyo ya Mbunge kuwathamini vijana, na kueleza kuwa inawapa hamasa kubwa ya kuendelea kupambana kujitafutia riziki, kwani sasa wanayo maeneo mazuri ya kujistiri wakati wa kiangazi na masika.


Mbunge wa Itwangi Azza Hillal Hamad akikata utepe kuzindua rasmi vituo vitatu vya bodaboda Tinde mara baada ya kuvijengea vibanda.











