
WATENDAJI wa vijiji, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Iringa wamepatiwa mafunzo na uelewa kuhusu utekelezaji wa Mradi wa INUA II unaotekelezwa na Hand in Hand Eastern Africa Tanzania (HIHEA), wenye lengo la kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia shughuli za uzalishaji na biashara.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa HIHEA, Jane Richard Sabuni, alisema taasisi hiyo imefungua rasmi ofisi yake mkoani Iringa na kuanza utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato kupitia vikundi vya ujasiriamali na biashara mbalimbali.
Alisema Hand in Hand imejikita katika kusaidia wananchi kuanzisha na kukuza biashara halali zitakazochangia kuimarisha uchumi wa kaya na kuboresha maisha ya familia. Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo tayari imewafikia zaidi ya wananchi 87,000, kusaidia kuanzishwa kwa biashara zaidi ya 50,000, kupitia vikundi zaidi ya 4,000 vya kiuchumi vilivyoundwa na kuimarishwa, na kuchangia kuzalishwa kwa ajira zaidi ya 74,000 nchini.
Sabuni alisema semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo viongozi wa serikali za vijiji na kata ili waweze kuelewa malengo ya mradi na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake, huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi wa serikali za mitaa ni muhimu katika kuhakikisha Mradi wa INUA II unafanikisha malengo yake ya kuimarisha uchumi wa wananchi.



