` SHILATU AZINDUA MASHINDANO YA KUSAKA VIPAJI KANDA YA KUSINI

WANDAMAN HOTEL

SHILATU AZINDUA MASHINDANO YA KUSAKA VIPAJI KANDA YA KUSINI

  

Emmanuel Shilatu 

Na Mwandishi Wetu

Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha sanaa na michezo vinakuwa nyenzo muhimu za ajira, maendeleo na ustawi wa vijana nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Ndugu Emmanuel Shilatu wakati akimwakilisha Mkuu wa Wilaya katika hafla ya uzinduzi wa Mashindano ya Kusaka Vipaji vya Sanaa na Michezo kwa Watoto kutoka mikoa ya Kanda ya Kusini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Shilatu alisema Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi kupitia ushirikiano na wadau wa michezo na sanaa.

"Serikali imeweka vipaumbele vyake katika kuendeleza vipawa na vipaji vya wanafunzi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo na sanaa. Hivi karibuni Serikali imeboresha mfumo wa elimu ili kuwaandaa vijana kujifunza amali mbalimbali, ikiwemo michezo na sanaa, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea," alisema Shilatu.

Kwa upande wake, mratibu wa mashindano hayo kutoka Shirika la Compassion International alisema jukwaa hilo limeandaliwa kwa lengo la kuwapa watoto na vijana fursa ya kuonyesha vipaji vyao, kujifunza, kujijengea kujiamini na kuandaa mustakabali bora wa maisha yao.

Alisema mashindano hayo yatazingatia misingi ya haki, nidhamu, ushindani wa afya pamoja na kutoa burudani yenye viwango vya hali ya juu kwa washiriki na watazamaji.

Naye mmoja wa wazazi wa washiriki, Bi. Prisca Richard, alieleza kufurahishwa na uwepo wa kambi hiyo ya kusaka vipaji, akisema ana matumaini makubwa kuwa kipaji cha mwanae kitazidi kukua na kumsaidia kutimiza ndoto zake za baadaye.

Mashindano hayo yameandaliwa na Shirika la Compassion International na yanawakutanisha washiriki pamoja na timu kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 26, 2026, ambapo mgeni rasmi wa hafla ya kufunga anatarajiwa kuwa Waziri wa Vijana, Mhe. Joel Nnauka.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464