` SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MIKUTANO YA HADHARA YA VYAMA VYA SIASA

WANDAMAN HOTEL

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MIKUTANO YA HADHARA YA VYAMA VYA SIASA


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kusimamisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa kwa kipindi cha sasa, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa wananchi na kudhibiti vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge leo, Katambi alisema Serikali imeongeza umakini katika masuala ya ulinzi baada ya kubaini viashiria mbalimbali vya vitendo vya uhalifu, ikiwemo ukamataji wa watu wanaodaiwa kujihusisha na silaha haramu pamoja na mipango ya uhalifu katika maeneo tofauti nchini.

Kutokana na hali hiyo, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimepewa maelekezo ya kuongeza doria na ulinzi katika maeneo yanayoonekana kuwa katika hatari, huku viongozi wa mikoa na wilaya wakitakiwa kuhakikisha Kamati za Ulinzi na Usalama zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litachukua hatua kali dhidi ya biashara au shughuli zozote zitakazobainika kukiuka sheria au kuhatarisha usalama wa wananchi, ikiwemo kuzifungia kwa muda pale itakapobainika kuwa ni muhimu kufanya hivyo.
Katika hatua nyingine, Katambi amewataka wamiliki wa hoteli, nyumba za wageni, Airbnb na malazi mengine yote kuhakikisha kila mgeni anayefikia katika maeneo yao anasajiliwa kwa kutumia kitambulisho halali cha NIDA au nyaraka nyingine zinazotambulika kisheria.

Ameonya kuwa wamiliki watakaoshindwa kutekeleza wajibu huo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na taasisi binafsi ni muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464