` HUDUMA ZA DHARURA HOSPITALI YA KOLANDOTO KUIMARIKA BAADA YA KUPOKEA VIFAA TIBA VYA SH MILIONI 279.2

WANDAMAN HOTEL

HUDUMA ZA DHARURA HOSPITALI YA KOLANDOTO KUIMARIKA BAADA YA KUPOKEA VIFAA TIBA VYA SH MILIONI 279.2

 

Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Tanzania, Mussa Masanja Magwesela akipokea maelezo ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi ICU katika hospital ya kolandoto
Katika hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani, Hospitali ya Kolandoto imepokea vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya shilingi milioni 279.2 kwa ajili ya Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU), ikiwa ni sehemu ya jitihada za hospitali hiyo kuboresha huduma na kufikia hadhi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Vifaa hivyo vimekabidhiwa kupitia Huduma ya Mana chini ya uongozi wa Wachungaji Christopher Mwakasege na Dayana Mwakasege, kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya na kuimarisha uwezo wa hospitali katika kuhudumia wagonjwa wenye hali mbaya wanaohitaji uangalizi maalumu.
"Vifaa hivi ni uwekezaji katika maisha ya watu, vinakuja wakati muafaka ambapo hospitali inaendelea kupanua uwezo wake wa kutoa huduma za kibingwa na huduma za wagonjwa mahututi," amesema Magwesela.

Aidha, amebainisha kuwa Huduma ya Mana imeendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kijamii katika kuboresha sekta za afya, elimu na maendeleo ya jamii, huku akisisitiza umuhimu wa wadau kuendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha huduma za afya nchini.

Akizungumza wakati wa ibada ya kuweka wakfu vifaa hivyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Tanzania, Mussa Masanja Magwesela, amesema msaada huo ni mchango mkubwa katika safari ya maendeleo ya hospitali hiyo kuelekea kuwa Hospitali ya Rufaa ifikapo mwaka 2030.
Naye Askofu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Zakayo Bugota, amesema kanisa linaendelea kufuata taratibu na vigezo vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha Hospitali ya Kolandoto inapanda hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Amesema upatikanaji wa vifaa hivyo ni moja ya hatua muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu na kukidhi mahitaji ya msingi yanayotakiwa kwa hospitali inayolenga kutoa huduma za rufaa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kolandoto, Joseph Sahani, amesema hospitali hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa na huduma katika kitengo cha wagonjwa mahututi, licha ya kuwa moja ya hospitali kongwe na muhimu katika ukanda huo.

Sahani amesema kwa sasa hospitali inaendelea na maboresho makubwa ya miundombinu ya jengo la ICU pamoja na vitengo vinavyohudumia watoto wachanga, hususan wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti), ili kuhakikisha huduma za dharura na za uangalizi maalumu zinapatikana kwa kiwango cha juu zaidi.
"Vifaa hivi vitasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi zaidi kwa kuongeza uwezo wa madaktari na wauguzi kutoa huduma za haraka, salama na zenye ufanisi. Ni msaada mkubwa wenye tija kwa hospitali na jamii kwa ujumla," amesema Sahani.

Hospitali ya Kolandoto, yenye historia ya zaidi ya miaka 113, imeendelea kuwa moja ya taasisi muhimu za utoaji wa huduma za afya mkoani Shinyanga na kanda ya ziwa kwa ujumla, Kwa miaka mingi, hospitali hiyo imehudumia maelfu ya wananchi na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya afya katika eneo hilo.

Kupokelewa kwa vifaa hivyo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha huduma za wagonjwa mahututi na kuongeza uwezo wa hospitali kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya, huku ikiendelea kutekeleza maono yake ya kuwa hospitali ya rufaa inayotoa huduma bora, salama na zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa

TAZAMA PICHA KATIKA MATUKIO MBALIMBALI

👇 👇👇👇























Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464