
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini na Mwanahabari Mkongwe, Dk Samwilu Mwafisi, amesisitiza kuwa hakuna nchi inayofurahia uhuru wa habari kwa asilimia mia moja, kwani uhuru huo daima unafungamanishwa na mazingira maalum ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kisheria ya taifa husika.
Anasema ni makosa makubwa kutumia vigezo vya nchi za Magharibi kupima hali ya tasnia ya habari barani Afrika bila kuzingatia vigezo vya ndani na matakwa ya jamii zetu.
Dk Mwafisi amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari wa gazeti la serikali HabariLeo kuhusu uhuru wa vyombo vya habari huku mashirika ya kimataifa yakitoa ripoti na tathmini zinazoainisha viwango vya uhuru huo.
Hata hivyo, wataalamu wengi wa mawasiliano wanabainisha kuwa tathmini hizo mara nyingi zinashindwa kuakisi uhalisia wa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania. Katika muktadha huo, Changamoto kubwa inajitokeza pale ambapo mataifa yanayoendelea yanapokubali kuwekewa vigezo vya nje ambavyo mara nyingi havijali mazingira yao ya ndani.
Mtazamo huu wa kijumlajumla unaziweka nchi nyingi za Afrika katika madaraja ya chini, ingawa kiuhalisia zinaweza kuwa na viwango vizuri vya uhuru wa habari vinavyoendana na mazingira yao ikilinganishwa na mataifa mengine.
Dk Mwafisi amesema katika utendaji wa kila siku, tasnia ya habari inakabiliwa na mifumo mbalimbali ya udhibiti ambayo inaathiri namna wataalamu wanavyowajibika kwa jamii. Kuna udhibiti wa ndani wa uhalisia ambao unahusisha kanuni na taratibu rasmi za taasisi ambazo kila mfanyakazi anapaswa kuzifuata anapoingia kazini ili kulinda malengo ya chombo husika.
Ili vyombo vya habari viweze kuleta manufaa halisi kwa jamii, kuna haja ya kujenga uhusiano imara na wa kitaaluma kati ya serikali na wanahabari, unaoongozwa na misingi ya ukweli.
Waandishi wa habari nchini Tanzania wanapaswa kujiamini, kuepuka uoga wa kufikirika, na kutekeleza wajibu wao kwa weledi mkubwa.
Alisema uhuru wa habari haupaswi kuwa wa rula moja kwa mataifa yote, bali unapaswa kujikita katika uwajibikaji unaozingatia mazingira halisi ya nchi ili kuwasilisha habari zenye ukweli, uaminifu, na manufaa ya kudumu kwa maendeleo ya jamii.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464