Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Frank Nkinda, amezindua rasmi eneo la utalii wa ikolojia katika Msitu wa Lubaga (Hashi), uliopo Manispaa ya Shinyanga, huku akitaja hatua hiyo ni fursa muhimu ya kuendeleza vivutio vya ndani na kukuza uchumi.
TAZAMA VIDEO👇👇
Uzinduzi huo umefanyika leo Juni 27, 2026, ambapo ulienda sambamba na kutembelea kujionea vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya msitu huo.
Nkinda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amesema sekta ya utalii ni moja ya nguzo kuu zinazochangia ukuaji wa uchumi wa nchi, na kwamba Auwepo wa mradi huo utafungua fursa mpya za kiuchumi mkoani humo.
Aidha, amewapongeza wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kwa ubunifu wa kuanzisha utalii wa ikolojia katika msitu huo wa Lubaga, akibainisha kuwa mbali na kukuza uchumi, utasaidia pia wananchi kupata maeneo tulivu ya kupumzika na kuimarisha afya zao za akili.
Naye Afisa Mwandamizi wa uhifadhi wa Misitu kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga Fabian Balele, amesema lengo la kuanzisha utalii wa ikolojia katika eneo hilo, ni kusogeza huduma hiyo karibu na jamii ili kuwawezesha wananchi kujionea na kujifunza kuhusu mambo ya asili.
Balele amefafanua kuwa, katika eneo hilo kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwamo utalii wa picha, maeneo kufanyia mazoezi, kuendesha baiskeli, mapumziko ya kifamilia, utalii wa nyuki, kambi za kulala na kuota moto msituni, pamoja na maeneo maalum kwa ajili ya hafla na kufunga ndoa.
"Katika mwaka ujao wa fedha wa serikali, tumejipanga kuuendeleza zaidi msitu huu ikiwa ni pamoja na kuanzisha bustani maalum ya wanyama (zoo) ili kuongeza mvuto kwa wageni," amesema Balele.
Kwa upande wao baadhi ya wadau wa maendeleo mkoani humo, akiwamo Frola Kajumla wameipongeza TFS kwa hatua hiyo ,huku wakibainisha kuwa mradi huo utakuwa mkombozi mkubwa kwa wafanyakazi, katika kutuliza akili na kukabiliana na tatizo la afya ya akili, na pia itakuwa sehemu nzuri ya kupumzika na familia.
MAELEZO KATIKA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akizungumza.
Mwakilishi wa Kamanda wa Kanda TFS Aloyce Nkilemwa akizungumza.
Afisa Mwandamizi wa uhifadhi wa Misitu kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga Fabian Balele akizungumza.
Katibu Tawala wa wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akizungumza.
uzinduzi ukiendelea wa utalii wa ikolojia msitu wa Lubaga.